HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 30, 2023

Bashe: Ni kweli bei ya vyakula imepanda

 Na Janeth Jovin 


Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema ni kweli bei ya mazao ya chakula imepanda kutokana na changamoto nne zilizoikabili serikali ya awamu ya sita tangu iingie madarakani.


Waziri Bashe ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zuhura Yunus akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya ziara mbalimbali alizofanya Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.



Bashe amesema kupanda kwa bei ya vyakula imetokana na mabadiliko tabianchi, vita ya Urusi na Ukraine, Uviko 19 na kupanda kwa gharama za mafuta.


Hata hivyo Bashe amewaonya watanzania kujiepusha na matapeli huku akisisitiza kuwa hakuna kilimo cha mitandaoni bali mtu anayetaka kulima ni lazima aende moja kwa moja shambani.



Bashe amesema hakuna kilimo kinachoendeshwa kwa njia ya WhatsApp, Instagram wala Twitter hivyo watanzania wasidanganyike na matapeli waliopo mitandaoni.


"Mliopo mjini mtambue kuwa hakuna kilimo kinachoendeshwa kwa WhatsApp, Instagram wala Twitter msidanganyike, ni kweli watu wengi wanaibiwa tumeshashughulikia ishu kadhaa, sasa tunamfuatilia mtu mmoja anaitwa Mr Kuku kwani tumeshapokea malalamiko mengi kama wizara," amesema Bashe na kuongeza


"Acheni kulima kwa WhatsApp na Twitter, hakuna mtu anaweza kukuambia lete milioni 10 baada ya miezi mitatu utapata Milioni 15, niwaombe ndugu zangu kwenye kilimo, hakuna njia ya mkato kama una hela yako kanunue ardhi ajiri kijana wa Chuo Kikuu muweke shambani msimamie zalisha, acheni kabisa wengi wanaibiwa," amesema


Naye Yunus amesema kuhusu ziara ya Rais Dk. Samia nchini Uswizi na Senegal zimezaa matunda kwani Rais 

alifanya mazungumzo na mwigizaji maarufu wa filamu duniani kutoka Uingereza Idris Elba na mkewe ambao  wameonesha nia ya kufungua studio hapa nchini kwa ajili ya filamu.



Yunus amesema mazungumzo hayo ndio kwanza ameanza lakini yakifanikiwa studio hiyo itakayojengwa itaweza kusaidia sio tu Tanzania lakini Afrika Mashariki na kati kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Pages