HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 21, 2023

Dully Sykes kufungua Pazia Tamasha la Bongo Fleva Honors


Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

MSANII wa mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Abdul Sykes 'Dully Sykes' atafungua pazila la Tamasha litakalofanyika kwenye Kituo Cha Utamaduni Cha Ufaransa 'Alliance Francaise' Upanga Dar es Salaam Januari 27 mwaka huu.

Dhumuni la tamasha hilo ambalo limepewa jina la Bongo Fleva Honors ni mahusus kwa wasanii wakongwe kuwakumbusha na kuwapa burudani wadau na mashabiki wa muziki huo waliyoikosa kwa kipindi kirefu.

Katika shoo hiyo ambayo itafanyika kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi, msanii mkongwe atakayepanda jukwaani atafanya show  live kwa kupigiwa vyombo na vyombo na Swahili Blues. 

Pia katika kila onesho msanii atakayekuwa siku hiyo historia yake itasimuliwa tangu kuanza kwake muziki hadi alipo sasa na nini anafanya kwa kipindi hiki na mipango yake endelevu kupitia sanaa hiyo na mambo mengine.

"Madhumuni makubwa ya Jukwaa hili la Bongo Fleva Honor zaidi litatumika kutambua na kuheshimisha muziki wa wakongwe wa Bongo Fleva na kuwapa fursa mashabiki wa enzi hizo kujikumbusha na kupata burudani ambayo wameikosa kwa muda mrefu huku wakiwa bado na kiu ya kusikiliza ngoma hizo," amesema Joseph Mbilinyi 'Sugu' wakati akimtambulisha Dully Sykes.

Baada ya kutambulishwa mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Dully Sykes ambaye alitambulika kwa mashabiki wa muziki huo kupitia ngoma ikiwamo 'Nyambizi',Shikide' 'Hunifahamu', 'Inde', 'Ladies Free', 'Baby Candy', 'Dhahabu Funga' 'Domo Lako', 'Hi', 'Kabinti Special', 'Salome', 'Nampenda Yeye', 'Action'  na nyinginezo amesema ni furaha kwake kupata heshima ya kuwa wakwanza kufanya onesho hilo litakalofanyika kila mwezi.

"Namshukuru Sugu kwa kunichagua kua wa kwanza kufanya onesho katika mfululizo wa matamasha yajayo yatakayohusisha wasanii wengine wakongwe, kwangu ni historia na heshima kubwa naahidi kufanya makubwa siku hiyo kikubwa Mungu aniamshe salama na ninawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi," amesema mkongwe huyo ambaye yupo kwenye 'game' kwa zaidi ya miaka 20.

Katika mfululizo wa matamasha hayo ambayo yameandaliwa na Msanii nguli, 'Sugu' kupitia timu yake ya Deiwaka World kwa kushirikiana na Kituo Cha Utamaduni Cha Ufaransa na Kampuni ya Paisha inayojishughulisha na Huduma ya Tax Mtandaoni na Usafirishaji wa Chakula na Vifurushi kwa wateja wao, zitasaidia kuondoa 'gap' kati ya wasanii wa zamani na sasa na mashabiki wa zama mpya watapata fursa ya kuona wakongwe mbalimbali na kufuatilia historia ya muziki huo kupitia ratiba ya kila mwezi.

Pia Kiongozi wa  Bendi ya Swahili Blues, Leo Kanyia kwa upande wake amesesma kuwa wana uzoefu wa kutosha wa kufanya live show kwani wameshafanya na wasanii wengi wa ndani na nje hivyo wameahidi kufanya show ya hali ya juu na ya kimataifa.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Utamduni cha Ufaransa nchini Tanzania, Flora amesema kuwa kiingilio cha maonesho hayo yatakayofanyika kila mwezi kitakuwa Sh 20,000 kwa kila onesho.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Paisha inayojishughulisha na Huduma  ya Tax Mtandaoni  Usafirishaji ,Abraham Lesulie, amesema kuwa wameona kua sehemu ya historia kwao kushirikiana na mkongwe wa muziki huo Sugu kufanikisha maonesho hayo na zaidi kutokana na kuvutiwa na wazo hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages