NA MWASHAMBA JUMA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaagiza watendaji wa taasisi za Umma kutekeleza kwa wakati maagizo yote yanayotolewa na Serikali ili kujenga ufanisi wa majukumu yao.
Dkt. Mwinyi alitoa maagizo hayo wakati akifungua Mkutano wa tano wa Baraza la Taifa la Biashara Ikulu, Zanzibar.
Alisema ameunda taasisi ya Ofisi ya Rais ya Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini, (PDB) ili ifuatilie mambo yote yanayoamuliwa na Serikali kwa nia ya kuyapatia suluhisho kwa wakati uliokubaliwa.
“Nimeunda taasisi hii lengo ni kufuatilia utekelezaji wa mambo yote tunayoyaamua serikalini” Alisisitiza Rais Mwinyi.
Alisema Uchumi wa Zanzibar unakabiliwa na changamoto mbalimbali licha ya kuendelea kuboreka na kueleza kuwa baadhi ya changamoto hizo ziko ndani ya uwezo wa Serikali kwaajili ya kuzitatua na baadhi yao ziko nje ya uwezo kutokana na sababu za kiulimwengu.
Rais Dk. Mwinyi alisema, athari za ugonjwa wa COVID 19 ziliathiri sana uchumi wa dunia na mataifa mengi kutetereka kiuchumi haswa uchumi wa nchi za visiwa ikiwemo Zanzibar.
Alisema licha ya ugonjwa huo kupungua na kumalizika kwa baadhi ya mataifa lakini bado umendelea kuyaandama mataifa mengine ikiwemo China ambae ni Mshirika mkubwa wa Maendeleo kwa Uchumi wa Zanzibar.
Aliongeza sekta ya usafirishaji bidhaa ni moja ya changamoto inayohujumu uchumi wa dunia kutokana na sababu mbali mbali za kidunia na kueleza kuwa Zanzibar kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na changamoto hiyo mbali na ufinyu wa bandari ya Malindi, unaodhorotesha huduma kwenye eneo hilo.
Akitoa ufafanuzi juu ya ujenzi wa bandari ya Mpigaduri, Dk. Mwinyi alieleza, Serikali ya awamu ya nane baada ya kuingia madarakani ilikuta tayari hatua za ujenzi wa bandari hiyo zilikamilika kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya makontena pekee nakueleza kuwa Serikali ya awamu ya nane iliona haja ya mahitaji yaliyopo kwenye bandari ya Malindi hayakidhi haja, ndio maana ilikuja na wazo la ujenzi wa bandari ya Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao utakwenda kuondosha changamoto zote.
“Wakati serikali ya awamu ya nane inaingia madarakani, ilikuta tayari mpango wa ujenzi wa bandari ya Mpigaduri ulikuwepo kwaajili ya kuanzisha bandari ya makontena pekee, hatua ya ujenzi huo ilifikia pazuri, lakini sisi tukaona tuzungumzie ujenzi wa bandari kubwa wenye kukidhi haja zote” alifafanua Dk. Mwinyi.
Alisema Zanzibar kwasasa inahitaji bandari yenye kukidhi haja zote ikiwemo bandari ya Makontena, bandari ya mafuta, bandari ya Samaki na bandari itakayotoa huduma za kubeba mizigo ya nafaka ikiwemo mchele na mambo mengine yenye uhitaji mkubwa, na kueleza kwamba Mpigaduri pekee isingetosha.
Alisema Serikali imefanya uamuzi wa ujenzi ya bandari ya Mangwapwani kutokana na kukidhi kwa eneo kwaajili ya mahitaji yote pia alieleza kina kirefu cha bahari kwa eneo hilo kinakidhi haja ya ujenzi na kuongeza kuwa Mpigaduri kutasaidia mahitaji ya bandari ya Malindi ambayo kwasasa imezidiwa kutokana na ufinyu wa nafasi na msongamano mkubwa wa huduma zinazotolewa.
Dk. Mwinyi alifafanua ujenzi wa bandari ya Mangapwani utashirikisha sekta binafsi na kueleza kwamba hautojengwa kwa fedha za mikopo.
Wakati huo huo Rais Dk. Mwinyi alizitaka Mamlaka za ulinzi ikiwemo Wizara yenye dhamana na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Kusimamia utendaji wa Polisi Utalii kwa kuwafunza juu ya kuwachunguza watembeza watalii na kuhakikisha kuwa wanavibali halali vya kutembezea wageni kwaaajili ya usalama wa watalii, mali na maisha yao pamoja na kuwaondoshea bugudha wageni.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati za Baraza la Taifa la Biashara, Katibu wa Baraza hilo ambae pia ni Katibu Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi, Mhandisi Zena A Said alieleza baraza lina kamati nne ambazo ni Kamati ya Uchumi na Biashara, Uwekezaji na Kulipa kodi, Kamati ya Kilimo Ufugaji, Uvuvi na Mazingira, Kamati ya Utalii na Kamati ya masuala ya Ardhi.
Mhandis Zena alieleza Baraza lilifanikiwa kuzifanyia kazi kwa kuzipatia ufumbuzi hoja mbalimbali zilizowasilisjwa na kamati hizo miongoni mwao alieleza ni Maslahi ya wanaopoteza ajira kwenye taasisi binafsi, Udhibiti wa wanaotembeza watalii wasiorasmi, Udhibiti wa nyumba za kulala wageni, Maegesho ya magari yanayotumia VAT, Athari za michezo ya baharini na Madai ya wakulima wa mbogamboga kwa uchelewashwaji wa madeni yao kwa taasisi za Serikali.
Aidha, Mhandisi Zena alieleza bahadhi ya mafaniko yaliyotokana baada ya kufanyiwa kazi kwa hoja za kamati hizo alisema Kuanzshiwa kwa Fao la ukosefu wa ajira kupitia marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, (ZSSF) nambari 5 ya mwaka 2005, Kutungwa kwa Sheria ya Mfuko wa huduma za Afya, Kuanzishwa kikosi cha Polisi Utalii na Diplomasia, Kuanzishwa kanuni za kusimamia nyumba za kulala wageni, Kuanzishwa mfumo wa ofisi Mtandao, Kuandaliwa mwongozo wa mahusiano baina ya wakulima na wamiliki wa mahoteli Pamoja na kuundwa kwa bodi ya ushauri ya masuala ya ajira na mishahara
Mkutano wa tano wa Baraza la Taifa la Biashara uliofunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri wa Serikali, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi wa taasisi za Serikali na Sekta binafsi.
Aidha, mada mbalimbali ziliwasilishwa kwenye mkutano huo ikiwemo Muhtasari wa Sheria ya Baraza la Taifa la Biashara la Zanzibar, Nafasi ya sekta binafsi katika kuchochoea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na nyengine ambazo zilichangiwa na wajumbe waliohudhuria mkutano huo.
No comments:
Post a Comment