HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 09, 2023

CUF chamtaka Jaji Biswalo aachie ngazi kufanikisha Tume ya Uchunguzi wa Fedha za Umma

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Chama cha Wananchi CUF kimesema, kazi ya kuchunguza na kutazama nini kimetokea na nini kiliharibu Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na kupelekea sehemu ya fedha za umma kutojulikana zilikowekwa haitoweza kufanikiwa kutekelezwa kwa uhuru na TUME iliyoundwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iwapo aliyekuwa Mkurugenzi wa Ofisi hiyo kipindi cha Plea Bargaining; Jaji Biswalo Maganga bado anashikilia nafasi ya juu katika moja ya ofisi ya utoaji haki, yaani Mahakama Kuu.

 


Akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba amesema Rais kubadilisha Mkurugenzi wa ofisi hizi peke yake hakutotosha kumaliza mizizi inayopelekea kujitokeza kwa mapungufu haya ya kiofisi, hivyo ili kuhakikisha ofisi hizi zinabadilika kabisa na kutekeleza majukumu yake kwa Muktadha wa Misingi ya Kikatiba, Demokrasia, Haki sawa kwa wote na Utawala bora kwa mujibu wa sheria, basi hata wale watumishi waliokuwa wakimsaidia Mkurugenzi wa Mashtaka kwa kipindi hicho cha “Plea Bargaining” wasimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi huru wa TUME hiyo na uchunguzi wake utakuwa wenye tija na kufuata Utawala wa Sheria pamoja na kurejesha imani ya Watanzania katika ofisi husika.

“Ndugu wanahabari, kama mtakumbuka “Plea bargaining” ililetwa na mabadiliko ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai yaliyofanyika mwaka 2019 na kuendeshwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kuingia makubaliano na Watuhumiwa wa makosa ya jinai ambao wengi wao hawakuwa wamepewa dhamana kutokana na makosa yao kutokuwa na dhamana. Hata hivyo sheria hii ilitekelezwa na DPP hata kabla ya Mhe. Jaji Mkuu kutunga kanuni za namna bora ya kutekeleza utaratibu wa “Plea bargaining” ambao ungeainisha mambo muhimu kama akaunti ipi ambayo fedha hizi zipelekwe na kuweka wazi namna ya matumizi ya fedha hizi. Jambo la kusikitisha zaidi, sehemu ya fedha hizi zilipokelewa na DPP mwenyewe kwa njia ya fedha taslimu kinyume cha sheria za nchi na zingine kuwekwa katika akaunti nchini China kama alivyoeleza Mhe. Rais” Amesema Profesa Lipumba.

Aidha amesema Tume pia ichunguze na kubainisha kama kuna viongozi na taasisi nyingine zilizohusika katika sakata hilo pamoja na uchunguzi wa fedha zilizopokelewa taslimu na zilizowekwa kwenye akaunti za benki, pia Tume ichunguze mali zisizohamishika zilizowekwa kama dhamana kwa wale walioshindwa kulipa fedha taslimu, kama bado ziko mikononi mwa Serikali au zimerejeshwa kinyemela.

Amebainisha kuwa wale watakaobainika wamehusika katika sakata hili ama la upotevu wa fedha au matumizi mabaya ya ofisi husika basi wachukuliwe hatua za kisheria ili kuzuia matukio kama haya kujirudia tena kwani wanaamini Tume itafanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, bila woga wala upendeleo.

Itakumbukwa kuwa, Tarehe 31 January, 2023 Mheshimiwa Rais alizindua Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki ikiwemo taasisi ya Taifa inayosimamia na kuendesha mashtaka ya jinai nchini. Wakati wa uzinduzi huu Rais Samia alinukuliwa akielezea juu ya kutoonekana kwa sehemu ya fedha zilizokusanywa kutokana na makubaliano kati ya waliokuwa watuhumiwa wa makosa ya jinai na Mkurugenzi wa Mashtaka yaani “Plea Bargaining” na kuripotiwa kwa kuwepo kwa akaunti ya benki nchini China ambako baadhi ya fedha hizo ziliwekwa huko.

No comments:

Post a Comment

Pages