SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesaini makubaliano ya ushirikiano kibiashara na Shirika la Posta na Mawasiliano la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiwa ni pamoja na kunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Kigoma, Tanzania kwenda hadi Kalame, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hafla hiyo ya makubaliano imefanyika leo jijini Dar es Salaam kati ya viongozi wakuu wa mashirika ya pande zote mbili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania, ikiwa ni kuendeleza ufanisi kiuchumi na kibiashara wa miundombinu ya Taifa ya Mawasiliano.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini ya makubaliano, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Peter Ulanga amesema shirika hilo limeingia makubaliano ya kushirikiana na Shirika la Posta na Mawasiliano la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mradi wa kunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka Kigoma nchini Tanzania kwenda Kalame, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiwa ni umbali wa kilometa 150-160 kupitia Ziwa Tanganyika.
"...Kutokana na ukubwa wa mradi huu, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo hii tunasaini mkataba wa makubaliano ili kushirikiana katika kukamilisha mradi huu kwa ufanisi. Mradi huu ni muhimu sana kwa nchi zetu kwani utafungua njia za mawasiliano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na nchi jirani kama Kenya, Uganda, Malawi, Msumbiji na nje ya Bara la Afrika. Pia mradi huu utaiwezesha Tanzania kifika nchi za Pwani ya Magharibi kupitia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo," alisema Bw. Ulanga.
"Nichukue fursa hii kuwahakikishia Shirika la Posta na Mwasiliano la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa, Tanzania ni moja kati ya nchi mbili Afrika zenye uwezo wa kuunganisha Bahari ya Hindi na Bahari ya Atlantiki kwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Pia tunayo miundombinu madhubuti ya mawasiliano na Serikali makini na wezeshi hivyo ni matarajio yetu kuwa mradi huu utafanikiwa," aliongeza Bw. Ulanga.
Aidha aliishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya Mhe. Nape Moses Nnauye kwa miongozo na ushirikiano wa dhati maouonesha kwetu Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL.
Pamoja na hayo, Bw. Ulanga amelishukuru Shirika la Posta na Mawasiliano la Jamhuri ya Demokrasia ya kongo na wawakilishi wa Shirika kwa kufikia hatua ya kusaini mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kukamilisha mradi huo mkubwa wa kujenga miundombinu ya mawasiliano kwa maslahi mapana ya nchi zote mbili.
No comments:
Post a Comment