HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 24, 2023

Je sheria mpya ya watu wenye ulemavu itawahakikishia ustawi bora?

Licha ya jitihada zinazochukuliwa na taasisi binafsi na serikali kupiga vita vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, bado vinashamiri siku hadi siku.

Jambo la kusikitisha udhalilishaji huu pia upo kwa watu wenye ulemavu.

Wamekuwa wakiripotiwa katika matukio ya kubakwa au kupewa ujauzito na baadae watuhumiwa kukimbia.


 

Moja ya changamoto kubwa ni uwezo wao mdogo wa kufahamu jinsi ya kuripoti vitendo hivyo na changamoto nyengine za kisheria hasa wakati wa kutoa ushahidi.

Hata hivyo, jamii ina wajibu wa kusimama imara kuendelea kupiga vita vitendo hivyo ili waweze kuishi kama watu wengine.

 

Aidha, taasisi zilizoanzishwa kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu wakiwemo wenye ulemavu wa akili, zinapaswa kusimama kidete kutetea haki zao ili zipatikane kwa wakati kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wanawajengea uwezo kulingana na mazingira yao.

Majid Najim, Ofisa uhusiano na Mawasiliano wa Jumuiya kwa ajili ya Watu Wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar (ZAPDD), anasema jumuiya hiyo imeandaa mikakati imara kuhakikisha inasimamia changamoto zinazolikabili kundi hilo ikiwemo kuwapatia elimu ya ujasiriamali.

“Jumuiya yetu inashughulikia watu wenye ulemavu wa akili, hivyo tuliona kwamba kundi hili limesahaulika katka jamii na ndio kundi ambalo huathirika sana  na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, tuliandaa mikakati ili kuhakikisha tunawakomboa na tunafanikiwa,” anasema.

Aidha, anasema jumuiya hiyo hufuatilia kesi za udhalilishaji zinazowakuta wanachama wao ili haki ipatikane kwa wakati.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Jamila Mohmoud Juma, anasema udhalilishaji wa kijinsia kwa watu wenye ulemavu bado upo mkubwa.

“Hili ni kundi ambalo lilisahaulika kwa muda mrefu, hivyo  jitihada zinahitajika kuhakikisha wanafikiwa na elimu ili wapate haki zao kwa wakati,” anasema.

Anasema ZAFELA  inachukua hatua mbalimbali ikikiwemo kufatilia kesi za udhalilishaji katika hatua zote ili kuhakikisha haki zao zinapatikana.

Anasema sheria mpya ya watu wenye ulemavu itahakikisha mazingira rafiki kwa kundi hilo.

Aidha alifahamisha kuwa ni wajibu wa jamii kuwatunza watu wenye ulemavu wa akili ili na wao waishi kama watoto wengine.

Ashraf Saleh, miongoni mwa mzazi ambae anaishi na mtoto mwenye ulemavu wa akili, alisema wazazi wanapaswa kupaza sauti zao kuhakikisha wanawalinda watoto wao sambamba na kuwa karibu nao ili waweze kuwaondolea mazingira hatarishi.

Kaimu Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar, Bakar Omar Hamad, alisema wakati umefika wa kusimamia haki za watu wenye ulemavu ili haki zao ziwe sawa na wengine wasio na ulemavu.

 

Alisema jumuiya hiyo inachukua jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na wazazi kuhakikisha watoto waliodhalilishwa wanapatiwa huduma stahiki na watuhumiwa wanafikishwa katika vyombo vya sheria.

 

“Yapo madawati wa kijinsia ambayo lengo lake ni kuwasaidia watoto na wanawake wanaodhalilishwa wakiwemo watu wenye ulemavu,” anasema.

 Anasema mwamko mkubwa umepatikana kupitia kwa elimisha jamii juu ya kusimama katika utoaji wa ushahidi, hivyo jamii imekuwa na ushirikiano mzuri katika kupata ushahidi. 

Kwa upande wa mwanamtandao wa kupiga vita vitendo vya udhalilishaji, Fatma Ali, anawashauri wazazi wenye watoto wenye ulemavu kutoa ushirikiano kwa serikali linapotokea tukio la udhalilishaji.

“Mazingira yanayowazunguka watoto wenye ulemavu bado ni hatarishi hivyo tuendelee kuwasaidia na kuwajengea uwezo,” anasema.

“Waswahili walisema mbio za sakafuni huishia ukingoni hivyo kwa pamoja tunaweza kufanikisha kudhibiti na kukomesha udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu,” anasema Fatma.

 

Aidha, anaipongeza serikali kwa kutunga sheria mpya ya watu wenye ulemavu na kuiomba kusimama kidete kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa kwa vitendo ili kupunguza shida zinazowakabili watu wenye ulemavu.

 

No comments:

Post a Comment

Pages