HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 10, 2023

Kampeni ya Umebima yazinduliwa Zanzibar



Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibu, Idrissa Kitwana Mustafa (wa pili kushoto), na Mkuu wa Idara ya Bima wa Benki ya NMB, Martine Massawe wakipeperusha bendera kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya Umebima kwa Zanzibar. Kampeni hii inalega kuhamasisha ukataji wa Bima za aina mbalimbali kupitia matawi ya benki ya NMB. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Mjini, Rashid Simai Msaraka na Kulia ni Meneja wa Biashara wa Benki ya NMB Zanzibar, Naima Said Shaame.

 

Na Mwandishi Wetu

 

Mchakato wa elimu ya bima na uhamasishaji wa matumizi yake umezidi kunoga baada ya jana Benki ya NMB kuzindua tena kampeni ya Umebima hapa Zanzibar kuchagiza uelewa wa huduma hii muhimu katika maisha na ujenzi wa taifa.

 

Msimu wa tatu wa Umebima na uelewa wa huduma za bima zilizopo sokoni ulizinduliwa rasmi kitaifa wiki jana mkoani Mbeya.

 

Ikiwalenga hasa wananchi wa kawaida na kuzingatia mahitaji ya wafanyabiashara wadogo, shughuli ya jana ilifanyika Darajani Sokoni na kuhudhuriwa na watu wengi hasa wajasiriamali wa eneo hili la Unguja.

 

Wakati zoezi la uzinduzi likiendelea, wengi walionekana wakikata bima hasa ile ya TZS 10,000/- mahususi kwa wamachinga na zoezi hilo lilipamba moto baada ya hotuba ya mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Bw Idrissa Kitwana Mustafa.

 

Kiongozi huyo alitoa hamasa kubwa sana kuhusu umuhimu wa kuwa na bima huku akiipongeza NMB kwa ubunifu wake wa kampeni ya Umebima ambayo alisema ni fursa nzuri ya maendeleo.

 

“Kutokana na elimu mtakayoitoa, Zanzibar inaenda kubadilika. Ubunifu wenu NMB wa elimu ya bima kwa umma unaendana na maono ya Rais Dkt Hussein Mwinyi ya kuboresha mazingira ya biashara ambayo ni pamoja na usalama wa mali na maisha kwa ujumla,” Bw Mustafa alibainisha,

 

Aidha, alisema kinga ya bima kwa Zanzibar sasa hivi siyo kubwa sana lakini kutokana na NMB kujitolea kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kutatua changamoto hii, ana matumaini makubwa uwekezaji wake utaongezeka.

 

Awali, Mkuu wa Idara ya Bima wa benki hiyo, Bw Martine Massawe, alisema licha ya umuhimu wake kwa maisha na uzalishaji na wingi wa elimu zinazotolewa kwa sasa, bado muitikio wa watu kuweka bima ni mdogo kwa nchi nzima.

 

Bw Massawe alibainisha kuwa takwimu zinaonesha ni asilimia chache sana ya Watanzania ndio wanaotumia huduma za bima lakini kutokana na jitihada za NMB kupitia kampeni za Umebima, sasa hali hiyo inaenda kuwa historia.

 

“Sisi kama Benki ya NMB tunatamani kuona idadi hii inaongezeka na inafikia walau asilimia 50 ya watanzania wawe wanatumia huduma za bima mpaka ifikapo mwaka 2029/2030,” mtaalamu huyo wa benki wakala alimwambia mkuu wa mkoa.

 

“Na hilo ndilo lengo kuu la kuja na kampeni hii ambayo itakwenda kutoa elimu kwa njia mbalimbali kuhakikisha idadi ya Watanzania wanaoweka bima iwe ya mali, afya au maisha inaongezeka. Lengo letu lingine likiwa ni kuongeza mchango wa sekta hii ndogo ya fedha kwenye Pato la Taifa kutoka chini ya asilimia moja sasa hivi mpaka walau asilimia tatu mwaka 2029/2030,” Bw Massawe aliongeza.

 

Kwa upande wa Zanzibar, alisema Umebima 2023 litakuwa ni zoezi la mwezi mzima na uzinduzi wa jana wa kampeni hiyo ni mkubwa kuwahi kufanyika katika Visiwa hivyo.

 

Pia Bw Massawe aliiambia hadhara hiyo kuwa ni kutokana na kutambua umuhimu wa bima kwa Watanzania, ndio maana NMB ikaona ni vyema kuuza bima za makampuni mbalimbali katika matawi yake yote kwa wateja na hata wasio wateja wake.

 

Mkuu wa Wilaya Mjini, Bw Rashid Simai Msaraka, aliipongeza NMB kwa uzinduzi wake wa kimkakati wa kampeni ya Umebima Mkoani Mjini Magharibi kwani wakazi wake 850,000 ni asilimia 46 ya watu wote visiwani humo.

 

“Naipongeza sana NMB kwani kila siku mnakuja na jambao jipya linalowanufaisha wananchi na kampeni hii ni mfano mzuri wa hilo.”

No comments:

Post a Comment

Pages