Na Shamimu Nyaki
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ametoa rai kwa Halmashauri zote nchini kuzingatia matakwa ya Sera ya Michezo ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo.
Naibu Waziri Gekul, ametoa rai hiyo Februari 09, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Masasi, Mhe. Geofrey Mwambe aliyetaka kujua ni lini Serikali itaboresha Uwanja wa Mpira wa Boma uliopo Masasi kwa kiwango kinachofaa kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana wa Masasi.
"Kwa mujibu wa Sera ya Michezo ya mwaka 1995 ibara ya 1-4, Jukumu la ujenzi wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Taasisi, Mashirika na watu binafsi. Hivyo nitoe rai kwa Halmashauri nchini kuzingatia matakwa ya Sera hii," ameeleza Mhe. Gekul.
Mhe. Gekul amesisitiza kuwa Halmashauri nchini zinatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za michezo pamoja na kukarabati miundombinu na kujenga viwanja kama zilivyofanya Halmashauri za Ruangwa, Geita, Nyamagana na Bukoba.
No comments:
Post a Comment