HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 25, 2023

MADIWANI RUNGWE WAKUMBUSHWA KUSIMAMIA UTOAJI MIKOPO KWA WANAWAKE, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu ameshiriki katika Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Busokelo Wilayani Rungwe pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo.

Akitoa salamu za Serikali katika baraza hilo, Haniu ameishukuru Halmashauri hiyo kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo kwa ufanisi na kuagiza Wakandarasi ambao hawajamaliza hiyo kufanya hivyo kwa wakati ili wananchi wapate huduma stahiki na Kwa wakati.

Wakati huohuo, Haniu ameagiza Watalamu mbalimbali katika Halmashauri hiyo kukusanya mapato ya Serikali kwa bidii huku akiomba Madiwani kuendelea kumulika vyanzo vya mapato katika maeneo yao ili kusaidia kutekeleza Miradi mbalimbali ya Maendeleo.

Aidha, ameliomba baraza hilo kusimamia kwa ukaribu utoaji wa mikopo  ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ikiwa ni 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.

Haniu ameongeza kuwa mikopo hiyo hutolewa na Serikali ili kuinua kiwango cha pato kwa wananchi, hivyo Halmashauri haina budi kutoa kwa wakati na kusimamia urejeshwaji wake ili iwanufaishe na wengine.

Katika hatua nyingine DC Haniu ameeleza Serikali imekuwa ikihamasisha wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wenye umri wa kujiunga na elimu ya Msingi sambamba na kidato cha kwanza hivyo kila mzazi na jamii kwa jumla ina wajibu wa watoto wote wanaenda shule.

Wanafunzi wawasili shuleni Halmashauri ya Busokelo mpaka sasa  wanafunzi wa kidato cha kwanza wameripoti  kwa 92% na darasa la  kwanza 103%.

Aidha, ameshukuru shule zote zinazotekeleza zoezi la chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari na kuagiza wazazi wote  ambao hawajaanza kutekeleza zoezi hilo kuanza kufanya hivyo ili kuondoa udumavu na utapiamlo kwa wanafunzi na kuongeza ufaulu shuleni.

Migogoro ya Ardhi
Kuhusu migogoro ya Ardhi, Haniu amekemea migogoro inayoendelea katika ngazi ya kaya na Jamii na kuwa utatuzi uendelee kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa kuwashirikisha viongozi na Baraza la Ardhi.

Amesema "Migogoro mingi inatoka ngazi ya kaya ni vema suluhisho lake pia likaanzia ngazi ya kaya  badala ya kugombana na kuhatarisha amani katika jamii."



Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu ameongoza zoezi la kukabidhi pikipiki kwa Watendaji wa Kata 06 na Maafisa Ugani 40 wa Halmashauri ya Busokelo Wilayani Rungwe zikiwa ni jitihada za Serikali  kuongeza uzalishaji mali shambani, kukusanya mapato na uimarishaji wa utawala bora.

Akikabidhi pikipiki hizo, Haniu ameagiza Watendaji hao wa Serikali kuhakikisha wanazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuwaletea Maendeleo wananchi na kuwaondolea changamoto mbalimbali zinazowakabili hasa Vijijini."

No comments:

Post a Comment

Pages