HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 23, 2023

DC Ubungo: NMB ni madaktari wa changamoto za kifedha

 

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba (wa tatu kulia), akipeperusha bendera na Mkuu wa Idara ya Bima wa Benki ya NMB, Martine Massawe (wa tatu kushoto) kuashiria uzinduzi wa Kampeni ya Umebima kwa Kanda  ya Dar es Salaam. Uzinduzi huo umefanyika katika eneo la Stendi ya Simu 2000 jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Afisa Biashara Manispaa ya Ubungo, Geofrey Mbwana, Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi, Aikansia Muro (wa pili kushoto), Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Mbezi Louis, Ian Meena (kulia) na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard (wa pili kulia). (Na Mpiga Picha Wetu).

 

NA MWANDISHI WETU

 

BENKI ya NMB imezindua Kampeni ya siku 21 katika Kanda ya Dar es Salaam ya kutoa elimu na kuhamasisha jamii kutumia Huduma za Bima, iitwayo UMEBIMA na NMB, huku Mkuu wa Wilaya ya Ubungo (DC), Hashimu Komba akiitaja taasisi hiyo kuwa ni madaktari wabobevu wa changamoto za kifedha nchini.

 

Uzinduzi huo umefanyika jana katika Stendi ya Daladala ya Simu 2000 (Mawasiliano), Ubungo jijini Dar es Salaam, chini ya kaulimbiu isemayo: 'Bima Zote, Sehemu Moja, Wakati Mmoja,' ambako magari ya kampeni na watoa Huduma wa NMB watazunguka maeneo mbalimbali yanayounda Kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, DC Komba aliishukuru benki hiyo kuufanyia katika Wilaya yake aliyoitaja kama sehemu sahihi na kwamba Serikali itashirikiana vema na NMB kuifikia jamii na kuielimisha juu ya umuhimu na faida za bima mbalimbali zikiwemo za afya, nyumba, magari, biashara na vifaa vya ndani. 

 

"Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano na NMB katika kuhakikisha makundi mbalimbali hasa ya wafanyabiashara wadogo (Machinga), waendesha Bodaboda, wajasiriamali na jamii kwa ujumla wanaelimika na kujikatia bima ambayo ni muhimu kwa utatuzi wa changamoto za kifedha wakati wa majanga.

 

"Uwepo wa viongozi wa masoko, vyama na mashirikisho ya wafanyabiashara wilayani Ubungo, ni uthibitisho kuwa hapa mmeanzia kampeni mahali sahihi na wameisubiri na kuipokea kwa hamasa kubwa. 

 

"Niwaombe NMB, mjitahidi kuyafikia makundi yote na jamii kwa ujumla na niwahahakikishie Wana Ubungo na Watanzania wote, NMB ni madaktari wabobevu wa utatuzi wa changamoto za kifedha nchini. Watumieni kufanikisha malengo yenu ya kukua kiuchumi," alisema DC Komba, ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan akitokea Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

 

Licha ya kuishukuru NMB kwa namna inavyojitoa kuunganga mkono jitihada za Serikali katika kuyasapoti makundi maalum yakiwemo ya Machinga na Bodaboda, pia aliipongeza kwa matumizi sahihi ya Program ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambako imetoa mchango mkubwa wa kuboresha miundombinu ya elimu, afya na usaidizi wakati wa majanga na kuitaka iendelee kusapoti Sekta ya elimu ambayo inakadiliwa na upungufu wa madawati, baada ya Ujenzi wa madarasa mengi uliofanywa na Rais Samia. 

 

Awali akimkaribisha DC Komba, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, alisema UMEBIMA ni kampeni endelevu inayolenga kutoa elimu ya kuhamasisha jamii kutambua umuhimu na faida za Bima, ambayo inaendelea kwa siku 21 kwenye mikoa ya Dar na Pwani, ambako watavutia Watanzania kukata Bima na kunufaika nazo wakati wa majanga.

 

"Elimu ya Bima bado inahitajika kwa Watanzania walio wengi na kwa kuwa NMB tunalitambua hili, tukaona umuhimu wa kuja na kampeni hii, iweze pia kuwanufaisha wajue pia na namna ya kudai fidia zao za Bima," alisisitiza Donatus. 

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Bima wa NMB, Martine Massage, alisema benki yake imejidhatiti vya kutosha kuwafikia Watanzania wote popote walipo, wakipewa nguvu kubwa na kampuni 10 washirika wao wa masuala ya bima.

 

"Soko la bima Tanzania linakabiliwa na changamoto ya elimu kwa jamii kutambua faida na umuhimu wa Huduma za Bima. NMB tunathamini jitihada za Serikali, ambayo imeshawapanga vizuri wafanyabiashara kiasi cha kuweka wepesi na urahisi katika kuwawezesha kukata Bima kupitia matawi yetu ambayo yanapatikana katika kila Wilaya," alibainisha Massawe.


No comments:

Post a Comment

Pages