HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 11, 2023

MORO YA KWANZA KUTEKELEZA AGIZO LA RT

NA TULLO CHAMBO, RT

MKOA wa Morogoro umeendesha mashindano ya riadha ya vijana chini ya miaka 18 na 19 'U-18 na U-20' ili kupata timu ya Mkoa.


Tanzania mwaka huu inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Afrika Mashariki 'EAAR U 18 na U 20', yatakayofanyika jijini Dar es Salaam, Machi 10-11.

Katika kuelekea mashindano hayo, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), liliagiza mikoa yote Tanzania Bara kuendesha mashindano kuanzia ngazi ya wilaya na mikoa, ili kupata timu zitakazowakilisha katika mashindano ya wazi Taifa na hatimaye kupatikana timu itakayoleta ushindani.

Katika kutekeleza agizo hilo, Leo Februari 11 Mkoa wa Morogoro umefanya mashindano kwenye Uwanja wa Jamhuri, ambayo yamefana.

Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Morogoro, Omar Kibukila, amesema licha ya taarifa kuwa ya muda mfupi, wilaya nne zimeitikia na kufanikisha mashindano hayo.

Kibukila, alizitaja wilaya hizo kuwa ni Manispaa iliyoleta wachezaji 14, Mvomero Saba, Gairo watano na Moro DC sita.
 
Katibu huyo, aliushukuru uongozi wa serikali ya mkoa, kwa kusaidia kufanikisha mashindano hayo ambayo yameonyesha matokeo chanya kwa kushuhudia vipaji vipya vya riadha Morogoro.

"Nichukue fursa hii kumshukuru RAS kwa kutushika mkono katika hili, pia pongezi ziende kwa Ofisa Michezo Mkoa, maofisa michezo wilaya, viongozi wote wa timu na wachezaji kuwezesha kufanyika kwa mashindano haya," alisema Kibukila na kuongeza.

Pia nichukue fursa hii kuomba radhi kwa mapungufu yaliyojitokeza na kumkwaza yeyote kwa na na moja ama nyingine, kwani hatukuwa na lengo baya zaidi ya kujenga.
 
Katibu huyo, aliongeza kuwa baada ya mashindano hayo, kamati ya ufundi itatangaza majina ya wachezaji watakaounda timu ya Mkoa.

Mashindano ya wazi ya Taifa U 18 na U 20 yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Februari 25, ili kupata timu ya Taifa itakayoiwakilisha nchi kwenye EAAR na baadae mashindano ya Afrika Lusaka, Aprili mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages