Moja ya njia ya chini ya mapitio ya wanyama iliyopo katika Shoroba ya Tembo Kilombero ambayo inaunganisha kati ya hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na Nyerere.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiangalia Shoroba ya Tembo Kilombero ambayo inaunganisha kati ya hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na Nyerere.
Na Janeth Jovin, Mang'ula, Ifakara
JUMLA ya tembo sita wamekufa kwa kugongwa na treni katika reli ya Tazara iliyopo kijiji cha Magombela Wilaya ya Kilombero huku watu saba wamepoteza maisha kutokana na kuuawa na wanyama hao pindi wanapohama kutoka hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa kwenda ya Nyerere.
Hayo yalibainishwa wilayani Kilombero halmashauri ya mji wa Ifakara jana na Meneja wa Shoroba ya Tembo Kilombero ambayo inaunganisha kati ya hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na Nyerere kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Mpango wa Kuhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP), Joseph Mwalugelo.
Mwalugelo aliyasema hayo mbele ya waandishi wa hifadhi wa wanyamapori na utalii kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) waliofanya ziara ya siku nne katika shoroba hiyo kupitia mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tuhifadhi Maliasili chini ya usimamizi wa JET.
Alisema tembo na watu hao wamepoteza maisha kutokana na kukosekana kwa njia za chini za mapitio ya wanyama hasa tembo katika shoroba hiyo ya Kilombero inaunganisha hifadhi hizo mbili za taifa.
"Tembo wamekuwa wakigongwa na treni mara kwa mara kwa mwaka 2021 waligongwa wawili, 2022 wanne, kwa upande wa vifo vya binadamu, mwaka 2018 tembo aliua mtu mmoja, 2019 mmoja, 2020 mmoja, 2021 watu wawili na 2022 waliuawa wawili pia, matukio haya yanatokea sana katika vijiji vya Mang'ula A, Sole na Kanyenja," alisema Mwalugelo
Hata hivyo alisema ili kupunguza vifo hivyo vya wanyama na binadamu ni muhimu kujengwa kwa njia za chini za mapitio ya wanyama na kubuni mbinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ukuta wa umeme katika shoroba hiyo ya Kilombero ili kupunguza tembo kuingia kwenye vijiji na mashamba kisha kuleta madhara kwa wakulima.
"Tayari tulishatumia mbinu nyingi za kuzuia tembo kutoka kwenye hifadhi na kuingia vijijini kisha kuleta madhara kwa wakulima kwa kuweka taa za sola, mizinga ya nyuki, mabati pamoja na fensi ya harufu katika shoroba hii, sasa hivi tunapambana kutafuta fedha kujenga ukuta wa umeme katika mapitio yote ya wanyama kwenye shoroba hii ya Kilombero, " alisema Mwalugelo
Aidha Mwalugelo alisema tafiti zinaonesha kuwa tembo wanazidi kuwa huru zaidi na katika kipindi cha mwaka jana zaidi ya 25 walionekana wakipita kwenye shoroba hiyo na kusababisha uharibifu wa mazao katika vijiji vya karibu na kuzuia wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Good News iliyopo kijiji cha Sole kwenda shule.
Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Abel Peter alisema anayashukuru mashirika mbalimbali yaliyojtokeza kufadhili ujenzi wa njia hizo za chini kwa ajili ya mapitio ya tembo kwani zitasaidia kupunguza madhara yanayotokea katika vijiji pindi wanyama hao wanapohama kutoka hifadhi moja kwenda nyingine.
No comments:
Post a Comment