HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 28, 2023

TANBAT6 watoa vifaa vya shule, michezo kwa wanafunzi Afrika ya Kati


Na Mwandishi Wetu


KIKOSI cha Sita cha Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania (TANBAT6) kinacholinda amani Afrika ya kati kimeshiriki maadhimisho ya siku ya elimu na utamaduni nchini humo, kwa kutoa vifaa vya shule na  michezo kwa wanafunzi mbalimbali.



Akikabidhi vifaa hivyo hivi karibuni, Kamanda Msaidizi wa kikosi hicho,  Maj Kassimu Abdalah alisema lengo lao ni kuchangia maendeleo ya elimu nchini hapo pamoja na ukuaji wa vipaji vya watoto kupitia tasnia ya michezo.


"Mbali na kuweka mwili sawa, michezo husaidia kuchangamsha akili, hatua itakayowawezesha watoto kufanya vizuri darasani. Utoaji wa vifaa hivi ni mwendelezo wa kukundi cha TANBAT 6 kushiriki matukio mbalimbali ya kimaendeleo nchini hapa, ikiwemo maandalizi ya mafunzo juu ya kukuza kipato kwa vikundi vya wajasiliamali," alisema


Mkuu wa Elimu mkoa wa Beriberati nchini humo, Matri Jodani alipongeza jitihada za TANBAT6 zinazolenga kukuza maendeleo ya elimu na kwamba mchango huo umetolewa kwa wakati muafaka kwani pamoja na mambo mengine, kukuza vipaji vya wanafunzi ni moja ya vipaumbele vya mkoa huo.


"Nina furaha kubwa kwa kitendo cha ninyi walinda amani wa Tanzania kushiriki nasi katika tukio hili muhimu, vifaa hivi mlivyotupatia vitasaidia kuwaongezea ari watoto katika masomo yao lakini pia kupenda michezo,” alisema


Mchango wa kikosi hicho ulitokana na kutambua kwamba elimu ni ndio msingi wa maisha na vijana wakipewa elimu ni ukombozi na maarifa katika nyanja mbalimbali za maisha ndani ya Afrika ya kati.

No comments:

Post a Comment

Pages