HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 20, 2023

TMA yafafanua kuhusu kimbunga “Freddy”

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa ufafanuzi juu ya taarifa za uwepo wa kimbunga “Freddy” zinazosambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuzua taharuki.




Kupitia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 imepewa jukumu kisheria kufuatilia na kutoa tahadhali za hali mbaya ya hewa kwa jamii.

Taarifa hizi za hali mbaya ya hewa hutolewa kwa jamii pale tu zinapokuwa zimekidhi viwango na miongozo ya utendaji kazi.

Kwa takribani wiki sasa Mamlaka imekuwa ikifuatilia mwenendo wa kimbunga “Freddy” kilichopo kusini magharibi mwa bahari ya Hindi karibu na pwani ya Madagascar na kujiridhisha kutokuwa na madhara ya moja kwa moja kwa sasa kwa maeneo yaliyoko nchini kwetu.

TMA kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, imesema inaendelea kufuatilia kwa kina mwenendo wa kimbunga hiki na itatoa taarifa punde kutakapokuwa na haja ya kufanya hivyo.

Aidha, Mamlaka inapenda kuikumbusha jamii na umma kwa ujumla kuwa kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Namba 2 ya 2019 kwamba Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa taarifa za tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa na ni kosa kisheria mtu mwingine kufanya hivyo.

Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

No comments:

Post a Comment

Pages