Wizara ya Elimu imewakumbusha wamiliki wa Shule kutoingiza shuleni vitabu vyenye maudhui ambayo hayaendani na mila na desturi na utamaduni wa nchi yetu.
Vitabu hivyo vimekuwa na hadithi ambazo maudhui yake yanahatarisha ukuaji na malezi ya mwanafunzi na pia kupotosha mila zetu katika makuuzi ya watoto na watanzania kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Francis Michael amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubaini kuwa kuna baadhi ya shule ambazo zimekuwa zikiingiza na kutumia vitabu ambavyo maudhui yake yanakinzana maadili ya kitanzania.
Amesema ni vizuri wamiliki na waendeshaji wa shule wakafuata Waraka Na 4 wa mwaka 2014 uliotolewa na Wizara ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kuhakikisha kuwa vitabu vya ziada na kiada vinavyotumika katika shule vina maudhui yanayoendana na mila na desturi na utamaduni wa nchi yetu.
"Wamiliki na waendeshaji wa shule zote za Umma na binafsi zilizosajiliwa hakikisheni mnafuata naa kuzingatia waraka huo pamoja na miongozo inayosimamia elimu ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria na mpaka kufutiwa usajili shule," amesema Katibu Mkuu Michael
Amesema Wizara itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kusimamia utoaji wa elimu na kuhakikisha njia za ufundishaji na ujifunzaji zinazingatia ubora na maslahi ya nchi.
No comments:
Post a Comment