Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala (wa pili kushoto), akipokea mfano wa tiketi ya ndege kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa (wa pili kulia), wakati wa hafla ya kukabidhi tiketi 12 zilizotolewa na benki hiyo kwa ajili ya viongozi wa vyama vya mashirikisho ya wafanyabiashara wadogo 'Machinga' na Bodaboda wanaokwenda Kigali nchini Rwanda kwa ziara ya mafunzo ya uendeshaji wa shughuli zao. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogoro na kulia ni Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard. (Na Mpiga Picha Wetu).
NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imefadhili ziara ya siku nne ya mafunzo kwa Viongozi wa Vyama na Mashirikisho ya Wafanyabiashara Wadogo (Machinga) na Waendesha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, wanaoondoka nchini Jumatatu Februari 6, kwenda Kigali, Rwanda.
NMB imekabidhi tiketi 12 za kwenda na kurudi Rwanda kwa wajasiriamali hao 10 na viongozi wawili, watakaoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogoro na Katibu Tawala Msaidizi - Uchumi na Uzalishaji, Dk. Elizabeth Mshote.
Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam leo Februari 3, 2023, ambako Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa NMB, Benedicto Baragomwa, alimkabidhi tiketi hizo Mkuu wa Mkoa, Mhe. Amos Makalla, ambaye ni mbunifu wa wazo la kupeleka viongozi hao Kigali, kujifunza namna sahihi za kuendesha biashara zao na Sekta ya Usafirishaji wa bodaboda.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kuwaaga, RC Makala aliipongeza NMB kwa kukubali kufadhili safari ya viongozi hao wa makundi hayo muhimu katika mpango mkakati wake wa kuipandisha Dar es Salaam kutoka nafasi ya sita kwa usafi barani Afrika, kuwa namba moja - inayoshikiliwa na Kigali hivi sasa.
"Nilipotembelea Rwanda, nikashawishika kutuma wawakilishi wa kwenda kujifunza na nikawasilisha wazo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alilikubali na kulibariki. Bahati mbaya sikuwa na fungu la kufanikisha ziara yao. Nashukuru NMB ikalipokea hili na kufanya uwezeshaji huu ambao unaunga mkono jitihada za Serikali.
"Ni wazo lililokuwa linaunga mkono jitihada za Rais Samia ambaye alikutana na Machinga Ikulu na kupanga nao mikakati ya kuboresha mazingira ya utendaji kazi wao na kuleta tija kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Leo tunakabidhiwa tiketi na Jumatatu nitawasindikiza Uwanja wa Ndege mimi mwenyewe," alisisitiza Makala.
Aliwataka viongozi hao kuitumia vema ziara hiyo kwa kuhakikisha wanajifunza mbinu sahihi za uendeshaji shughuli katika mazingira yasiyokwaza Mamlaka na Jamii, sanjari na kuwa mabalozi wema watakaovutia Wanyarwanda nao kuja kujifunza katika maeneo mengine na kushirikiana nao kibiashara.
Kwa upande wake, Baragomwa alisema siri ya NMB kuitikia haraka maombi ya kuwezesha ziara hiyo ni udau mkubwa ilionao kwa maendeleo ya jamii, hivyo walilipokea ombi hilo kama jukumu lao la kuinyanyua kada hiyo ya Machinga na Bodaboda kibiashara na kiuchumi.
Mbele ya Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, Baragomwa akasisitiza kuwa benki yake inajivunia ushirikiano baina yao, Serikali na jamii, alioutaja kuwa umechangia faida kubwa ya Sh. Bilioni 429 kwa mwaka 2022, pato lililotanua fungu la Program ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kufikia Sh. Bilioni 6.2.
Alibainisha kuwa, kupitia ziara hiyo, viongozi hao watajifunza mengi nchini Rwanda, ambako nao wametuma wawakilishi wawili, huku akiwahakikishia huduma bora na rafiki pindi watakaporudi zikiwemo za NMB MastaBoda na mikopo yenye riba nafuu kwa Machinga na wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa.
Aidha, DC Mpogoro alimshukuru RC Makala kwa wazo lake hilo linaloenda kumaliza changamoto za kiutawala dhidi ya makundi hayo, huku Mwenyeviti wa Machinga Dar, Namoto Yusuph na wa Bodaboda Dar, Saidi Chenja, wakiiahidi NMB na Serikali kutumia ziara hiyo kwa ustawi wa shughuli zao na miundombinu ya Jiji na usafi wa mazingira.
No comments:
Post a Comment