HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 09, 2023

MADIWANI KYELA WAPONGEZA HUDUMA ZA AFYA KUBORESHWA


Mkuu wa wilaya Kyela, Josephine Manase akizungumza wakati akitoa salamu kwenye kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Kyela.

 Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya Kyela wakiwa kwenye kikao.

 

 NA DENIS MLOWE, KYELA

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Kyela mkoani Mbeya, limempongeza na kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuboresha huduma za afya katika hospitali ya wilaya na hivyo kuwaondolea adha na kero kubwa ambayo walikuwa wanakumba nayo wananchi wilayani hapa.

 

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Kyela, Katule Kingamkono, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akitoa taarifa kuhusu masuala ya afya wilayani Kyela ikiwa ni katika kikao cha baraza la madiwani kwa robo ya pili, Kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa halmashauri uliopo Kyela mjini.

 

Kingamkono alizitaja huduma zilizoboreshwa hospitalini hapo ni pamoja na vipimo vya mashine ya X-Ray ambavyo vilikuwa ni adha na kero kubwa kwa wananchi wilaya ya Kyela na kulazimika kutumia hospitali za mbali tofauti na sasa.

 

Alitumia kikao hicho kuwataka madiwani kufikisha habari njema kwa wananchi wa maeneo yao na kuwatangazia rasmi kwamba kwa sasa huduma bora za mashine ya kisasa ya X-Ray ambayo ni ya mfumo wa kompyuta tofauti na zile za zamani zinatolewa katika hospitali ya wilaya.

 

Aliongeza kuwa zamani wananchi walikuwa wanalazimika kusubiri wapigwe picha, Na kisha wasubirie waipepee picha ili ikauke ndipo iweze kusomwa taarifa zake lakini sasa hivi ni mfumo wa kompyuta ambao mgonjwa anaweza kujiangalia viungo vyake vyote vya ndani ya mwili wake.

 

"Nitumie nafasi hii kuwapa pole wananchi wote wa wilaya ya Kyela ndani na nje, ambao walipata adha na kero kubwa wakati walipokuwa wanaenda hospitali ya wilaya kupata huduma za kitabibu" alisema Kingamkono. alisema.

 

Aidha Mwenyekiti halmashauri alisema, katika eneo la afya ya kinywa na meno,wamepata vifaa vya kisasa sasa hata huduma ya meno bandia na uzibaji wa meno yaliyotoboka sasa hivi wanao uwezo wa kusafishwa kisha kuzibwa meno yao yaliyotoboka.

 

Kwa upande wa chumba cha kutunzia miili ya marehemu, Kingamkono alisema wameweza kupata jokofu lenye uwezo wa kutunza miili sita kwa wakati mmoja na pia chumba kimeboreshwa na sasa kina hali bora zaidi.

 

"Vile vile, tumefanikiwa kununua mashine ya kisasa ya kufulia nguo ambayo kwa wakati mmoja inao uwezo wa kufua mashuka 50 ambayo itatusaidia sana katika masuala ya usafi katika hospitali yetu ya wilaya Kyela" alisema Kingamkono.

 

Kingamkono alilitaja eneo lingine lililoboreshwa ni chumba kwa ajili ya kufanyia mazoezi, kwa wale wanaokutwa na changamoto ya ugonjwa wa kupooza sehemu ya miili yao hivyo kwa sasa wanacho chumba maalum kwa ajili ya kufanyia mazoezi.

 

Kwa upande mkuu wa wilaya Kyela, Josephine Manase, alisema ameridhishwa na usimamizi wa madiwani, katika miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa kwa kasi wilayani hapa na kutoa wito waendelee kusimamia kwa ukamilifu ili wananchi waweze kunufaika nayo.

 

 “Pamoja na kazi nzuri mnazoendelea kuzifanya, naomba nitilie msisitizo katika baadhi ya mambo ambayo nitaomba msaada wenu, kwa ajili ya kwenda kuyatekeleza katika maeneo yenu hasa hii miradi ya maendeleo ambayo ipo kwenye kata zenu” alisema Josephine.

 

Akizungumzia kuhusu suala la afya mkuu wa wilaya huyo mpya alisema vituo vya afya vikijengwa katika ubora, basi vitakaa kwa muda mrefu na watakuwa wanaokoa gharama za serikali katika kurekebisha miradi hiyo, badala ya kutenga fedha kwa ajili ya kufanya shughuli nyingine.

 

“Kwa hiyo naomba tuwe mabalozi, lakini pia tuwe mawakili wa kuhakikisha ile miradi inakamilika kwa wakati lakini pia kuhakikisha inakuwa na viwango vinavyotakiwa, kama mradi upo chini ya kiwango na wewe umepitia na kuiona kasoro hiyo, ni vyema tupeane taarifa…” alisema Josephine Manase.

No comments:

Post a Comment

Pages