HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 08, 2023

Nape: Serikali ipo tayari kupokea maoni ya wadau kuhakikisha mtandao unakuwa salama

Na Janeth Jovin 


TAKWIMU za kidunia zinaonesha kwamba ushiriki wa wanawake katika masuala ya teknolojia ni mdogo ikilinganishwa na wanaume na kwamba hali hiyo inasababishwa na changamoto ya usalama mitandaoni.


Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakati akifungua kongamano maalum la wanawake na teknolojia lililoandaliwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la The LaunchPad Tanzania.    


Nape amesema zipo jitihada kadhaa zinazofanyika ili kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo ya teknolojia ikiwemo ya Serikali  kuwa tayari kupokea  maoni  kutoka kwa wadau kuhakikisha mtandao unakuwa salama.


"Takwimu za dunia zinaonesha idadi ya wanawake na vijana hasa wanawake wanaoshiriki kwenye shughuli zinazotokana na TEHAMA sio nzuri kwani idadi ni mdogo  ukilinganisha na wanaume lakini zipo jitihada zilizokuwa zinafanyika kuona namna  ya kuongeza idadi ya ushiriki wao,” amesema.


Amesema ni ukweli uliyowazi kuwa waathirika wakubwa wa unyanyasaji mitandaoni ni wanawake hivyo kama Serikali wanawajibu wa kuchukua hatua kali ikiwemo ya kutunga sheria kadhaa ikiwemo ya kulinda taarifa binafsi kwa lengo la kuhakikisha mtandao upo salama ili kuwavutia wanawake kushiriki.


Nape amesema nchini takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 51 ya idadi ya watu ni wanawake hivyo wasiposhiriki  vya kutosha jamii kubwa ya Tanzania itakuwa haijashiriki katika Tehama.


"Tafiti zinaonesha wanawake wapo makini kwenye shughuli zao hivyo tukiwahamasisha wakashiriki katika masuala ya teknolojia kwa sehemu kubwa mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika jamii yetu yatapatikana, " amesema Nape nakuongeza


"Rais Samia Suluhu Hassan anawahakikishia kuwa Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri wa wadau wengine katika kuhakikisha mtandao upo salama  na kuwa eneo zuri la watu kufanya shughuli zao na kuhakikisha idadi ya wanawake inaongezeka  katika matumizi ya mtandao ili waweze kufanya shughuli zao za kila siku,” alieleza.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali  la The LaunchPad Tanzania, Carol Ndosi amesema kongamano hilo limejikita kufanya tathmini kama nchi imefikia wapi  katika safari ya wanawake na teknolojia, kuangalia fursa na changamoto wanazokutana nazo.


“Tumegundua takwimu tofauti tofauti ambazo  zinaonesha kuwepo na mwanya mkubwa katika matumizi  na kutengeneza teknolojia ambapo wanawake ni wachache na hawafahamiki,” amesema.


Carol amesema kupitia kongamano hilo wameiomba wizara husika kuangalia sera ya ICT kutokuwepo na kipengele kilichotaja wanawake, kupitia sheria itakayotoa uhakika wa usalama mtandao kwa wanawake ili kuweza  kuhamasisha ushiriki wao.


Naye Mshiriki wa  kongamano hilo, Mhandisi  Fatuma  Mwamba aliiomba serikali kuyafanyia  kazi mambo watakayojadiliana na kuyaingiza katika sera ya Tehama.

 

No comments:

Post a Comment

Pages