HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 08, 2023

RBWB yajinasibu kulinda, kuendeleza vyanzo vyake

 

Na Irene Mark, Iringa


MKURUGENZI wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB), Florence Mahay amesema licha ya changamoto ya uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji, wamejipanga vema kulinda na kuendeleza bonde hilo muhimu.



Alizungumza hayo leo Machi 6, 2023 mbele ya waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari wanaofanya ziara ya kujifunza na kuona shughuli za bonde hilo kwenye baadhi ya maeneo yake.


Alisema RBWB ni bonde la pili kuanzishwa kisheria hapa nchini likiunganishwa na mito mikuu minne ambayo ni Ruaha Mkuu, Luwegu, Kilombero na Rufiji yenyewe.


“Mto Ruaha unachangia asilimia 15 ya maji kwenye bonde letu la Rufiji, Kilombero ni mkubwa unachangia asilimia 62 wakati mto Luwegu unaingiza maji kwa asilimia 18 na Rufiji yenyewe ni asilimia tano tu.


“Hili bonde ni kubwa mno, maji yake yanapita kwenye mikoa 11 hapa nchini katika wilaya 34 na Halmashauri 45 kote huko kuna watu wanayatumia maji hayo kwa shughuli hasa za kilimo, ufugaji na kijamii.


“Ndio maana tunasema bonde la Rufiji linahitaji kulindwa kwa namna yeyote ile kuanzia kwenye vyanzo vyake na kutizamwa kwa jicho la kipekee,” alisema Mahay.


Mhaidrojia wa RBWB, Ally Diwani alisema ukubwa wa bonde hilo ni kilomita za mraba 183,791 sawa na asilimia 20 ya eneo la nchi hii.


Diwani alisema bonde hilo linachangia asilimia 15 ya  Pato la Taifa (GDP) kupitia sekta ya kilimo, ufugaji, nishati na utalii.


“Maji ya hili bonde ni muhimu sana kwenye ujazaji wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere kule Rufiji... na wote tunafahamu umuhimu wa bwawa lile kwenye uchumi endelevu wa taifa letu,” alisema Diwani.


Akizungumzia namna wanavyoishirikisha jamii katika utunzaji wa vyanzo na mito ya bonde hilo, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa RBWB, Upendo Lugalla alisema wanashirikiana na jamii kupanda miti na kuitunza.


Lugalla alisema wameanzisha Jumuiya 42 za watumia maji ikiwa ni mkakati wa miaka mitano tangu 2020 hadi 2025 lengo ni kuwa na jumuiya 120 za watumia maji kwenye bonde la Rufiji zenye jukumu kubwa la kutunza na kulinda hasa vyanzo vya maji.


“Tangu Desemba,2022 hadi Februari,2023  tumepanda miti 73,643 tukishirikiana na jumuiya za watumia maji, lengo ni kupanda miti zaidi ya 200,000 ifikapo Aprili mwaka huu,” alisema Lugalla.

No comments:

Post a Comment

Pages