Na John Richard Marwa
Wekundu wa Msimbazi Simba SC wametinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kuwanyuka African Sports ya Tanga kwa mabao (4-0) mtanange uliolindima Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jioni ya leo.
Simba waliingia kwenye mchezo huo wakitoka kucheza mechi ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL ugenini dhidi ya Vipers ya Uganda mtanange ambao Simba waliibuka na ushindi wa bao moja kwa bila.
Katika kikosi cha Mnyama leo kilichovaana na African Sports kulikuwa na mabadiliko makubwa kwa asilimia kubwa kutoka kikosi cha kwanza cha hivi karibuni huku akianza Jean Baleke na Pape Sakho tu kwenye kikosi hicho.
Beno Kakolanya, Esrael Mwenda, Gadiel Michael, Mohamed Outtara, Kennedy Juma, Jonas Mkude, Erasto Nyoni, Pape Sakho, Habibu Kyombo, Jean Baleke na Moses Phiri.
Licha ya mabadiliko hayo makubwa ya kikosi lakini Simba walionesha ukubwa wao kwa kushambulia kwa Nguvu licha ya African Sports kuweka ukuta wa maana hasa kipindi cha kwanza na kuwachukua Simba dakika 40 kuanza kuandikisha bao la kwanza kupitia kwa Jean Baleke akimalizia pasi ya upendo ya Pape Sakho.
Kipindi cha pili Simba walirejea kwa Nguvu na kuumaliza mchezo dakika ya 46 Kennedy Juma aliandikisha bao la pili akiunganisha kona iliyochongwa na Moses Phiri, kisha Mohamed Musa na Stephen Mwanuke wakamalizia misumali ya mwisho kwenye jeneza la African Sports.
Kwa ushindi huo unakuwa wa pili mtawalia kwa Mnyama Simba mara baada ya kupokea vipigo kwenye michezo miwili ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL kundi C ambapo Simba alipokea kipigo kutoka kwa Horoya AC ugenini kisha wakapoteza nyumbani Benjamin Mkapa dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco.
Ushindi huo kwa Simba ni rekodi bora msimu huu kwenye mashindano hayo ya ASFC kwa kushinda michezo yote mitatu kuanzia hatua ya 64 bora, wakimtoa Eagles kwa mabao (8-0) kisha wakaifurusha Coastal Union kwa bao (1-0) na leo African Sports kupokea dozi ya chuma (4-0).
Simba katika ASFC wameshinda michezo mitatu, wastani wa ushindi ni asilimia 100, wakiwa na clean sheet'3 na mabao 13 katika dakika 270.
Baada ya mchezo wa leo Simba wanaingia kambini kjiwinda na kibarua cha mchezo wa nne wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL kundi C ambapo Simba atawaalika Vipers Benjamin Mkapa Machi 7.
No comments:
Post a Comment