HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 08, 2023

VITENDO VINAVYOWAKIMBIZA WATOTO MAJUMBANI VYATAJWA


Bi Adventina Kyamanywa ambaye ni Mkuu wa Kituo cha kulelea watoto cha Tumaini Children's Center.

 

Na Lydia Lugakila, Bukoba

Ikiwa leo ni maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani Jamii Mkoani Kagera yatakiwa kupunguza vitendo vya ukatili vinavyowafanya watoto kukimbia majumbani mwao ikiwa ni pamoja na ugomvi kati ya wazazi, vipigo kwa watoto  wenyewe, kuchomwa Moto,  kubakwa na watu wao wa karibu pamoja na wazazi kushindwa kutimiza Majukumu yao.

Kauli hiyo imetolewa na Bi Adventina Kyamanywa ambaye ni Mkuu wa Kituo cha kulelea watoto kinachopatikana kata ya Nyanga Manispaa ya Bukoba kinachomilikiwa na Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi wakati akiongea na mtandao huu Ofisini kwake.

Bi Adventina amesema kuwa Kituo hicho kimekuwa kikipokea na kuwahudumia watoto waliopo katika Mazingira hatarishi waishio mitaani wanaofanya shughuli za kujitafutia pesa kama kukusanya makopo, vyuma chakavu, kuchota maji na kumwaga uchafu  huku akikiri kumpokea mtoto  mdogo aliyekimbia nyumbani kwao baada ya kuchomwa vidole vya miguu na Mama ake wa Kambo kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kudokoa wali.

Amesema wanapowapokeawatoto wa namna  hiyo kituoni hapo hukaa nao kwa karibu na kuwajengea Mazingira mazuri ya kupata taarifa zilizowakimbiza na baadae  kukutana na familia zao kusuluhisha baadhi ya kesi na kuwarejesha kwa wazazi wao huku akidai kuwa zipo kesi ambazo zinakuwa ni ngumu kwao zinazowafanya kuendelea kuwalea watoto ili wajitambue na kurudi shule.

"Jamii inatakiwa kupunguza vitendo vya ukatili vinavyowafanya watoto kukimbia majumbani kwani tunapata ugumu katika kulea wazazi wanatakiwa kujua kuwa wanapowakimbiza watoto waelewe kuwa mtaani kuna maisha magumu watoto wanakumbana na kazi ngumu zilizo chini ya umri wao na kufanyiwa vitendo vibaya zaidi" alisema Bi Adventina.

Hata hivyo ameiomba Serikali kuendelea kuweka Sheria ya   kuwawajibisha wanaotenda vitendo hivyo kwa watoto pamoja na wanaoshindwa kutimiza wajibu wao ili kupunguza vitendo vya ukatili.

No comments:

Post a Comment

Pages