HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 14, 2023

TIMU YA TAIFA U 20 & 18 YAKABIDHIWA VIFAA

NA TULLO CHAMBO, RT



UONGOZI wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), umekabidhi vifaa kwa Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 18 na 20 inayotarajiwa kushiriki mashindano ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika jijini Lusaka, Zambia, Aprili 29 hadi Mei 3 mwaka huu.


Vifaa hivyo, suti za michezo na viatu maalumu vya kukimbilia 'spikes', vilikabidhiwa na Makamu wa Rais RT, William Kallaghe, leo Aprili 13, mara alipotembelea kambi ya timu hiyo iliyopo kwenye hosteli za Baraza la Maaskofu (TEC), Kurasini jijini Dar es Salaam.


Vifaa hivyo, vilipokelewa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Alfredo Shahanga, mbele ya kikosi kizima cha timu hiyo.


Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Kallaghe, kwanza alianza kwa kutoa salamu za pole kwa familia ya michezo hususan Riadha, kutokana na kifo cha aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa RT, John Bayo, kilichotokea hivi karibuni na anayetarajiwa kuzikwa Ijumaa Aprili 14 jijini Arusha.


Baada ya salamu hizo, Kallaghe, alisema vifaa hivyo ni sehemu ya matakwa ya shirikisho hilo kwa timu hiyo inayokwenda kupeperusha bendera ya Tanzania huko Zambia.


"Tumetoa vifaa hivi ili kupunguza changamoto iliyokuwa ikiikabili timu na hii ni awamu ya kwanza, awamu ya pili ambayo imebaki kama viatu pair tano, tutaimalizia ndani ya siku mbili hizi," alisema Kallaghe na kuongeza.


Hii ni timu yetu ya Taifa, hivyo ni yetu sote, tunaendelea kuwaomba wadau mbalimbali kuendelea kutusapoti shirikisho katika programu zetu mbalimbali.


Aidha, Kallaghe, aliwataka wachezaji kuendelea kudumisha nidhamu ya kambi na kuzingatia mazoezi, kwani wana jukumu kubwa linalowakabili mbele yao.


Kwa upande wa Kocha Shahanga, alishukuru uongozi wa RT kwa vifaa hivyo, kwani changamoto ilikuwa kubwa kwa baadhi ya wachezaji kutokuwa na vifaa stahiki vya mazoezi.


Naye Nahodha msaidizi, Mwanaamina Mkwayu, alishukuru na kueleza kuwa vifaa hivyo vitawaongezea morali ya mazoezi.

No comments:

Post a Comment

Pages