Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona akipanda mche wa Mkonge katika Shule ya Sekondari Coastal jijini Tanga kuashiria uzinduzi wa Klabu ya Mkonge shuleni hapo jana.
Na Mwandishi Wetu, Tanga
BODI ya Mkonge Tanzania (TSB), kwa kushirikiana na Shule ya Sekondari ya Coastal ya jijini Tanga, zimezindua Klabu ya Mkonge kwa wanafunzi wa shule hiyo ambayo imelenga kuwafundisha vijana kuhusu kilimo cha Mkonge na Sekta ya Mkonge kwa ujumla hatua itakayowawezesha kujiajiri baada ya kumaliza masomo.
Akizindua klabu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Saddy Kambona amesema wazo la kuanzisha klabu hiyo lilizaliwa kwenye Mahafali ya kidato ya shule hiyo Machi mwaka huu, lakini baadaye ikaonekana isiwe klabu kwa ajili ya Shule ya Coastal pekee bali ianzishwe klabu itakayoshirikisha shule zote za Tanga na vizazi vinavyokuja kushiriki kwenye uchumi huu wa mkonge.
Amesema kwa muda mrefu imezoelekea kwamba elimu yetu haimuandai mwanafunzi kwenda kujitegemea anapomaliza shule, wengi wamekuwa na mtazamo kuwa kazi ya kuajiririwa ndiyo inafaa.
“Kwa hiyo sisi tulitazama wazo la kuwa na klabu za Mkonge kwa maana kama tunasema Mkonge ni Tanga na Tanga ni Mkonge, basi tunataka mtu akifika Tanga aone kweli kama Mkonge ni Tanga, tunategemea aone kwamba Mkonge ndiyo zao kuu la kibiashara.
“Yaani kuanzia anatua uwanja wa ndege anapotua anaona bidhaa za Mkonge barabarani hadi anapofika hotelini anakutana na mazuria ya mkonge na bidhaa nyingine.
"...Sasa sehemu ya kuanzia ni kuwa na klabu za kuhamasisha si tu kilimo cha mkonge bali pia kuhamasisha matumizi ya bidhaa za mkonge lakini pia kushiriki kwenye kuzalisha bidhaa hizo.
“Baada ya hayo sasa bodi inakuwezesha kupata elimu, utaalamu kuanzia shambani kulima Mkonge na uongezaji wa thamani, wataalamu wetu watatoa ujuzi huo kwa vijana wa Tanga na nje ya Tanga ili wanapomaliza shule huko wanakokwenda wakawafundishe na wengine,” amesema Kambona.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Zao la Mkonge na Masoko, Olivo Mtung’e, akizungumzia faida za mkonge na somo la kuhamasisha wanachama wa klabu hiyo alisema mahitaji ya mkonge kwa sasa yameongezeka ndiyo maana wanahamasisha wakulima kulima zao hilo.
“Nchi nyingi sasa zinahitaji mkonge lakini kiasi ambacho tunakilima kwa sasa ni kidogo ndiyo maana baada ya kuingia kwenye kilimo cha wakulima wadogo sasa tunahamasisha na sisi kwenye familia zetu wenye mashamba ya eka moja hadi tatu walime mkonge kwa sababu kwa sasa hali ya hewa inatusukuma kuelekea huko kwani zao la hili linahimili hali zote za hewa ili kuimarisha uchumi wa familia,” amesema Mtung'e.
Mkurugenzi Mtung’e anasema kutokana na hali hiyo, wahitimu hawana haja ya kutafuta ajira kwa sababu mkonge wenyewe ni ajira kwani ukishapanda baada ya miaka mitatu unaanza kuvuna hadi kwa muda wa miaka 18.
Kwa upande wake mwanafunzi wa shule hiyo na mmoja wa wanachama wa klabu hiyo, Fatuma Mshashi amesema klabu hiyo yenye wanachama 50 ambao kati yao wavulana ni 23 na wasichana 27, inatekeleza malengo mbalimbali ikiwamo kufanya tafiti kuhusu kilimo cha zao la mkonge ili kuona faida zake, kutoa elimu kwa wanafunzi wengine, walimu, wadau wa elimu kuhusu umuhimu wa zao hilo, kuhamasisha jamii kutumia bidhaa za mkonge, kuwaandaa wanafunzi ili kuja kuwa wataalamu wazuri na wabobevu katika zao la mkonge na nyinginezo.
“Ili kufanikisha malengo katika Klabu ya Mkonge katika shule yetu, tunaomba ofisi yako kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwalimu Mkuu itusaidie kukutanishwa na wataalamu wa zao la mkonge tupate elimu na ujuzi wa zao hili, kuwezeshwa klabu kuwa na shamba darasa ambalo litakuwa la kujifunzia hatua zote za uandaaji hadi uvunaji ambapo shamba hilo litakuwa mradi wa klabu,” alisema mwanafunzi huyo.
No comments:
Post a Comment