Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdulhaman Abdalah akiongea na wananchi katika ziara yake ya kuzitembelea wilaya zote za mkoa huo kukagua uhai wa Maendeleo na kuwashukuru kwa kumchagua.
Na Mashaka Mhando, Kilindi
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoani Tanga, kimemshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekelezwa miradi ya barabara mkoani hapa.
Akizungumza wakati alipotembelea ujenzi wa barabara ya Handeni-Kibirashi-Kiteto- Chemba-Kwamtoro hadi Singida, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdulhaman Abdalah alisema kuanzia Julai mwaka huu barabara hizo zitatengewa fedha.
Alizitaja barabara nyingine ni Tanga-Pangani hadi Bagamoyo ambayo ujenzi wake unaendelea na barabara nyingine ni ile inayotoka Handeni- Mziha hadi Tuliani ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
"Huyo ndiyo Dakitari Samia Suluhu Hassan, ninachowaomba ndugu zangu tumuunge mkono ifikapo mwaka 2025 mkoa wetu uongoze kwa kumpa kura nyingi," alisema Mwenyekiti huyo.
Awali akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Handeni kwenda Singida, mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa barabara mkoa wa Tanga, Mhandisi Jotrevas August alisema usanifu wa kina wa uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa mradi wote wa kilomita 434.33 uliofanywa na kampuni ya kihandisi ya M/s Inter-Consult kwa gharama ya shilingi milioni 710.497 mwaka 2017.
Alisema baada ya hapo utekelezaji wake kwa awamu ya kwanza ulianza Juni mwaka 2022 kiasi cha kilomita 20 kutoka Handeni hadi Mafuleta kwa gharama za sh 24,439,653,737.50 ukitekelezwa na mkandarasi wa kampuni ya Henan Highway Engineering Group ya China.
Hata hivyo, Mhandisi August alisema ujenzi huo wa kilomita 20 ulikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ucheleweshwaji wa fedha kwa wakati.
Alisema kazi iliyofanyika hadi sasa ni kwa kiwango cha asilimia 14.01 na kutakiwa kumalizika kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini kutokana na changamoto hizo bado hawajamaliza.
Akizungumza baada ya taarifa hiyo Mwenyekiti alisema ni kweli kulikuwa na changamoto hiyo lakini Rais Dkt Samia tayari amekubali kutoa fedha zote za mradi huo kuanzia Julai baada ya kutengewa bajeti yake yote.
Alisema barabara hiyo ambayo ni ya kimkakati ikikamalika itasaidia kusafirishia mizigo na mazao kwenda mikoa ya kati lakini pia itawasadia wafanyabiashara wanaotumia bandari ya Tanga.
Aliwaomba wananchi wamuunge mkono Rais kwavile amekuwa akijenga uchumi wa Tanzania kwa kutoa fedha katika miradi mbalimbali ambayo imekuwa na tija kwa nchi
"Rais amekuwa akihangaika kutafuta fedha huko na huko ka ajili yetu sisi wananchi, kazi yetu sisi ni kumuunga mkono tu basi ifikapo mwaka 2025," alisema Mwenyekiti huyo.
No comments:
Post a Comment