HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 18, 2023

MAKAMU WA RAIS AAGIZA UJENZI ZAIDI BARABARA ZA LOLIONDO

 

Makamu wa Rais Dakta, Philip Mpango akikata utepe kuashiria kufunguliwa rasmi kwa barabara ya Mto wa Mbu - Loliondo sehemu ya Waso –Sale KM 49 wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Muonekano wa barabara ya Mto wa Mbu - Loliondo sehemu ya Waso –Sale KM 49 wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

 

Na Mwandishi Wetu

 

Makamu wa Rais Dakta, Philip Isdor Mpango ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuanza kujenga sehemu ya tatu ya barabara ya Mto wa Mbu hadi  Loliondo KM 217,  (sehemu ya Ngaresero - Engaruka KM 39.2) ili kurahisisha huduma za usafiri, uchukuzi na utalii wilayani Ngorongoro.

Akizungumza wakati akifungua rasmi  barabara ya Mto wa Mbu - Loliondo sehemu ya Waso –Sale KM  49 , Dakta, Mpango amesema nia ya Serikali ni kuijenga na kuikamilisha barabara yote lakini kwa hatua ya sasa ni vema ikajengwa sehemu ya tatu mara baada ya kukamilika kwa sehemu ya kwanza.

“Najua kuwa mmeshaisanifu barabara yote toka Mto wa Mbu hadi Loliondo KM 217, sasa baada ya kumaliza sehemu ya kwanza ya Waso-Sale KM 49, hamieni sehemu ya tatu ya Ngaresero - Engaruka KM 39.2 kwa kuwa sehemu hiyo ina changamoto nyingi kwa wasafiri na wasafirishaji”, amesema Dakta, Mpango.

Ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha barabara kuu na za mikoa zinapitika wakati wote wa mwaka na kuwataka wananchi kuzitunza na kuzilinda ili zidumu kwa muda mrefu na kuleta tija kwa wafugaji, wakulima, wafanyabiashara na watalii na hivyo  kuchochea maendeleo.

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema Wizara itaendelea kuhakikisha inafanya matengenezo maalum ili sehemu ya pili ya Sale-Ngaresero KM 57.4 na sehemu ya nne ya Engaruka- Mto wa Mbu KM 60.9 nazo ziwe katika ubora na kupitika wakati wote wa mwaka.

Aidha amesema Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), umepanga kujenga kwa kiwango cha lami sehemu ya Waso-Loliondo KM 10 ili  kuunganisha na kuupendezesha mji wa Loliondo.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Rogatus Mativila  amesema barabara ya Waso –Sale KM 49 imejengwa na mkandarasi  China Wu Yi Co. Ltd kwa zaidi ya shilingi bilioni 87 na kukamilika kwake kutachochea ustawi wa sekta nyingine za kiuchumi hususan utalii,kilimo na ufugaji.

Makamu wa Rais Dakta, Philip Mpango yuko katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo  ya barabara, afya, mifugo, umeme, elimu, madini na maji mkoani Arusha.

No comments:

Post a Comment

Pages