HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 24, 2023

Prof Mbarawa: Tunawekeza kupata huduma, taarifa sahihi za hali ya hewa


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake bungeni leo Mei 22,2023.

 

 Na Irene Mark

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Mkame
 Mbarawa amesema serikali inaendelea kuwekeza kwenye ubora na utaalam kwa rasilimali watu ili kupata taarifa sahihi zaidi za hali ya hewa.

Profesa Mbarawa amesema hayo leo Mei 22,2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Alisema serikali imeboresha miundombinu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na inaendelea kuwekeza kwenye rasilimali watu ili kuongeza ufanisi na ubora ya shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo kwa maendeleo ya taifa.

"Tumewekeza kwenye miundombinu ya hali ya hewa ndio maana hata kiwango cha usahihi wa utabiri kimeongezeka hadi kufikia asilimia 94 kutoka asilimia 70 inayotambulika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani kutokana na ubora wa vifaa na miundombinu ya utabiri.

"Serikali imetekeleza mpango wa mafunzo kwa
watumishi 74 kati yao 64 waliendelea na masomo
na wengine 10 walihitimu mafunzo katika vyuo
mbalimbali ndani na nje ya nchi.

"...TMA pia inafanya tafiti mbalimbali za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi, jumla ya tafiti nne
zilichapishwa katika majarida ya kimataifa ya
kisayansi duniani," alisema Profesa Mbarawa.

Alisema TMA imeendelea kutoa, kusimamia, kudhibiti na kuratibu utoaji wa huduma za hali ya hewa hapa nchini zikiwemo taarifa za kila siku, siku 10 na ule wa muda mrefu.

Mamlaka pia inatoa tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa na kusambaza kwa
wananchi ili kuhakikisha usalama wa watu na mali zao na kuchangia katika kuimarisha utendaji wa
shughuli za kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, TMA pia imeendelea kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa, kufanya tafiti za kisayansi za hali mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na  kubadilishana taarifa za hali ya hewa katika mtandao wa dunia (Global Telecommunication System — GTS) kulingana na
makubaliano ya kimataifa.

Alisema TMA imeiwakilisha nchi katika mikutano 56 ikiwemo mkutano
wa 15 wa watumiaji wa data na huduma zitolewazo na Shirika la EUMETSAT Barani
Afrika, uliofanyika Dar es Salaam.

Aliliambia Bunge kwamba
watumishi 18 walishiriki katika semina 25 za
mafunzo ya hali ya hewa na kujengewa uwezo wa utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini.

Profesa Mbarawa alisema imekamilisha ukarabati wa Ofisi za hali ya hewa za Mahenge na Songea zikiwemo nyumba
tatu za wafanyakazi zilizopo Mahenge.

Alisema TMA inatekeleza mifumo ya udhibiti wa ubora katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa usafiri kwa njia ya maji, uendeshaji wa kituo maalum cha kanda kilichopo Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa miongozo ya utabiri wa hali ya hewa kwa nchi zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Mamlaka pia imepanua wigo na kuongeza ufanisi wa kufikisha huduma za hali ya hewa kwa wananchi
kwa kuongeza idadi ya redio, luninga na magazeti yanayotoa matangazo ya hali ya hewa na elimu.

Hadi kufikia Aprili, 2023, taarifa za hali ya hewa zinatolewa katika luninga 14 na vituo 86 vya redio na magazeti mawili.

No comments:

Post a Comment

Pages