HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 23, 2023

ZHC YAJIPANGA KUJENGA NYUMBA ZA BEI NAFUU UNGUJA, PEMBA

Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) limesema lina mpango wa kujenga nyumba za kuwapangisha watu wenye kipato cha chini katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.            
                                                                                                                                      
Kauli hiyo imetolewa mwisho wa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mwanaisha Ali Said wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Shirika hilo Darajani, Unguja.    
 

Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetenga ardhi ya akiba kwaajili ya Maendeleo hivyo Shirika litatumia fursa hiyo kujenga nyumba za kupangisha na  kuuza kwa wananchi mbali mbali  kwaajili ya kuleta makaazi bora.         
                                                                                                    

Mkurugenzi Mwanaisha  amesema  ZHC kwa sasa imeanza  kujenga nyumba za kuuza katika eneo la Mombasa kwa Mchina lakini hata mwananchi mwenyewe kipato cha chini anaweza kununua kutokana na utaratibu mzuri ambao ZHC  imepanga kuziuza nyumba hizo.
                                                                                            

Alieleza kwamba nyumba hizo zitauzwa kwa Wazanzibari waliyopo ndani na nje ya nchi,  muhimu mtu  afuate taratibu za manunuzi zilizoekwa na Shirika hilo.        
                                                                                                                                                           

Alifahamisha ZHC itauza nyumba hizo kwa njia tatu, aidha njia kulipa pesa zote kwa pamoja,  au njia ya kulipa pesa kwa awamu nne au kwa njia ya benki (mogeji hauzi).
                                                     

 "Morgage house  ni njia ambayo mtu anazungumza na benki hivyo sisi Shirika tunapokea pesa kutoka benki na lakini mteja yeye atafunga mkataba na benki kwaajili ya kukatwa pesa za nyumba hiyo" Alisema Bi Mwanaisha.
                                                                                             

Aliezea kwamba ZHC iko tayari kupokea pesa za nyumba zinazojengwa  Mombasa kwa Mchina kwani ujenzi umeshaanza tangu Machi 2023 na utamalizika baada ya miezi 15 kuanzia mwezi huyo.                
                                                                                                                                        

Amesema nyumba hizo zitauzwa bei tofauti kutokana na idadi ya vyumba kwani kuna nyumba za vyumba viwili zitauzwa tsh. Milioni 136 na nyumba ya vyumba vitatu zitauzwa milioni 153, bei hizo bila vati (VAT).   
                                                                                                                   

Aidha Mkurugenzi Mwanaisha alizungumzia suala la usafi wa mazingira katika eneo la nyumba hizo, alisema dhamana ya usafi, ZHC itamkabidhi Bodi ya Kondominia ambayo ni taasisi moja wapo ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi  ndio itakayobeba dhamana  ya kuweka Mazingira safi katika maeneo ya nyumba hizo. 

                                                                                  
Mkurugenzi Mwanaisha amemshukuru Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kuwaunga mkono katika gharama za Ujenzi wa nyumba hizo  kwani bila ya kupata msaada kutoka Serikali kuu Shirika lisingeweza.    


                                                                                     

Ujenzi wa Nyumba za Mombasa kwa Mchina utagharimu Tsh. Bilioni 9.8 ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa Tsh bilioni 6.8 na Shirika la Nyumba Zanzibar ( ZHC) limetoa Tsh Bilioni 3.

 

No comments:

Post a Comment

Pages