Na Lydia Lugakila, Bukoba.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bi Fatma Mwassa ametangaza neema kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo Machinga, Maafisa usafirisha maarufu Boda boda pamoja na Mama lishe Mkoani humo kwa kuhakikishia mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kufanya biashara zao bila vikwazo huku baiashara nyingine zikitarajiwa kuboreshwa na kutangazwa vyema ili kuuzika nje ya Nchi.
Bi Fatma Mwassa amebainisha hayo katika kikao na wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo Machinga, Boda boda na Mama lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Mkoa huo.
RC Mwassa amesema kuwa anaamini kuwa kundi hilo kwa namna yake limekuwa likifanya kazi kubwa na nzuri ikiwemo kuweka mzunguko wa biashara ndani ya Mkoa huo hivyo lazima Serikali ihakikishe inaweka Mazingira bora kwao na kuzitangaza vyema.
"Sasa tumefungua milango Mimi ni Mama yenu na nyie ni Wanangu nimekuja Kagera kufanya kazi tuendelee kushirikiana na suala la fedha kutoka Halmashauri itatoka kwa wakati na sisi kama Serikali tutaongeza mafunzo kwenu ili biashara zifanyike vizuri zaidi" alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali utaendelea kutengeneza miundo mbinu rafiki katika maeneo ambayo wajasiliamali watapangiwa ili waendelee na majukumu yao vizuri.
Ameongeza kuwa atataka kuanza na kundi la wauza senene ambapo amewahakikishia kuwa kuna mkakati unaadaliwa wa kubuni mtambo utakaorahisisha ukusanyaji wa senene bila usumbufu wala moshi ili kuwavutia watumiaji walioko nje ya nchi.
"Tutaangalia namna nyingine ya kuweka Mazingira wezeshi na kuboresha biashara ili iendelee kukua mwaka hadi mwaka na naahidi kuwa umachinga utakuzwa na kuendelezwa katika viwango vya juu" alisema Bi Fatma Mwassa.
Awali akisoma taarifa ya kazi zilizofanywa na shirikisho la umoja wa Machinga Mkoa wa Kagera (SHIUMA) Bi Husna Mohamed ambaye ni katibu wa Shirikisho hilo amesema kuwa Mkoa wa Kagera una jumla ya Wanachinga laki 1 na elfu 918 ambapo wanakabiliwa na Changamoto mbali mbali ikiwemo usafiri kufikia ngazi ya mitaa, Vijiji, kata na Wilaya ili kuratibu shughuli za Machinga pamoja na kutofanyika vikao na mikutano.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara hao akiwemo Johanitha Issack, Advela na Paschal wamesema kuwa kwa sasa wanakabiliwa na tatizo la mitaji, bidhaa zao kukosa Tbs, huku mmoja wa waendesha Pikipiki akiiomba Serikali kuwasaidia Boda boda kuondokana na mikataba umiza ya waajiri na kuwaweka katika hatua ya kupata unafuu katika marejesho kutoka Serikalini.
Hata hivyo Rc fatma amewahakikishia kwamba watapata mitaji kidogo kidogo kwa kuanzia kubwa ni kuwa na ofisi nzuri, kuwa wabunifu kwani fursa za biashara ni nyingi ambazo zinaweza kufanya matokeo makubwa na tofauti.
No comments:
Post a Comment