HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 23, 2023

Waziri Dkt. Biteko awaita Wadau kushiriki Kongamano la Madini na Uwekezaji



Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

WAZIRI wa Madini Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa wadau wote waliopo kwenye Sekta ya Madini nçhini Tanzania, Bara la Afrika na Ulimwenguni kote kushiriki Kongamano la Madini na Uwekezaji litakalofanyika Oktoba 25 hadi 26 Mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Dkt. Biteko ametoa kauli hiyo leo jijini humo katika Mkutano wa Uzinduzi wa Kongamano hilo linalojulikana kama Tanzania Mining Investment ambalo lengo lake ni pamoja na kuwasilisha taarifa muhimu za Sekta ya Madini, kuwa na vikao vya mazungumzo na wawekezaji.


Malengo mengine ni kubainisha fursa zilizopo kwenye miradi ya Madini, na kuimarisha ushirikiano wa ndani na nje ya Nchi katika kukuza na kuifanya Sekta ya Madini Tanzania kuwa endelevu.


“Kwa heshima na taadhima ninayo furaha kubwa kuwakaribisha kwenye mkutano huu wa Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini na pia naomba nichukue fursa hii kuwakaribisha wageni waalikwa katika uzinduzi wa leo. Nawakaribisha sana Tanzania kwani kwa sasa ni miongoni mwa Nchi zenye Mazingira mazuri ya kuvutia Uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja,” amesema Dkt. Biteko.


Waziri Dkt. Biteko amebainisha kuwa Tanzania ni moja kati ya Nchi zilizopo Afrika Mashariki, ambayo inakisiwa kuwa ni kitovu cha uzalishaji na uendelezaji wa Madini mkakati na muhimu yanayotumika kutengeneza vifaa vitakavyosaidia matumizi ya nishati safi.


Kwamba Tanzania inavutia wawekezaji mbalimbali kutoka Ulimwenguni kote kutokana na uwepo wa utajiri wa Madini ya aina mbalimbali, sera rafiki na ongezeko kubwa na uhitaji wa nishati endelevu.


“Tanzania imebarikiwa kuwa na Madini mkakati muhimu yanayohitajika katika uzalishaji wa magari ya umeme, miundombinu ya nishati mbadala na teknolojia nyingine zinazozalisha nishati safi,” ameeleza Dkt. Biteko.


Ametaja miongoni mwa madini mkakati na muhimu yanayopatikana Tanzania ni lithiam, Kobalti, Nikel, Graphite, na Madini muhimu.


Waziri Dkt. Biteko ameeleza kuwa Madini hayo yamekuwa na thamani kubwa kutokana na mwelekeo wa kidunia katika uendelezaji wa uchumi unaozingatia uzalishaji Mdogo zaidi wa hewa ya ukaa (low Carbon economy).


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ocean Business Partners Tanzania Ltd, Abdulsamad Abdulrahim amesema Kongamano hilo litawavutia zaidi ya watu 2000 kutoka Nchi zaidi ya 25 Ulimwenguni na litaambatana na mkutano utakao hodhi zaidi ya  wazungumzaji 100.

No comments:

Post a Comment

Pages