Na John Marwa
MENEJA Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba Ahmed Ally ametoa hisia zake juu ya Kiungo Maridadi Jonas Mkude ikiwa ni siku kadhaa tangu taarifa ya kuwa hatakuwa kwenye kikosi cha Wanalunyasi msimu ujao kutolewa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita klabu ya Simba ilitoa taarifa ya kuwa kiungo huyo hatakuwa sehemu ya kikosi mara baada ya mkataba wake kuisha.
Ilikuwa taarifa iliyopokelewa kwa taswira tofauti tofauti na wadau wa mpira wa miguu nchini kutokana na jina la Mkude na ukubwa wake akiwa mchezaji aliyekaa klabuni hapo kwa miaka 13.
Mapema leo Meneja Habari na Mawasiliano Ahmed Ally ametoa hisia zake kupitia ukurasa wake wa 'Instagram' akionyesha kuguswa na namna wanasimba watakavyo mkumbuka 'Nungu Nungu' Jonas Gerald Mkude.
"Muda umetenganisha mapenzi yetu na Jonas Mkude. Ameondoka mtu tunaempenda kweli, ameondoka Mtoto wetu, mtoto wa nyumbani kwetu Kwa miaka ya hivi karibuni hakuna mchezaji tumewahi kumpenda kama Jonas Mkude na tutaendelea kumpenda.
"Wakati Simba ina njaa, Azam ilimhitaji hakuenda, UTO walimtaka hakuenda akachagua kuvumilia njaa yetu huyu ni zaidi ya mchezaji kwetu.
"Sisi tulitamani Jonas Mkude amalizie mpira wake Simba kwani hatutaki kucheza nae akiwa timu nyingine Kwa sababu tukimfunga ataumia na yeye akitufunga ataumia hatuko tayari kumuumiza Mkude wetu.
Tumetoa taarifa ya kuachana nae punde tutatoa taarifa ya kumuaga na tutamuaga kwa heshima zote. Sisi ndo tunatambua zaidi heshima ya Mkude kuliko mtu mwingine yeyote na tutamuaga kwa heshima hiyo hiyo. Kila la heri Legend" ameandika Ahmed.
Mkude anaondoka ndani y Mitaa ya Msimbazi, zizi lililomlea na kukitabulisha kipaji chake cha Soka akiwa na mataji 16 ya michuano mbalambali ikiwemo Ligi Kuu Soka Tanzania Bara NBC PL mara tano. Huku kimataifa akiifikisha Simba hatua ya Robo Fainali mara tatu Ligi ya Mabingwa na mara moja Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
No comments:
Post a Comment