HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 23, 2023

JET yaita wadau udhibiti viumbe vamizi, migogoro

Exuperius Kachenje

Serikali na wadau wa uhifadhi mazingira wameshauriwa kuongeza nguvu ya ushiriki wa pamoja katika kudhibiti viumbe vamizi wanaoathiri mazingira, jamii na uchumi sanjari na migogoro ya wanyamapori na binadamu.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Mazingira(JET), Dk. Elle Otaru jijini Dar es Salaam Juni 21, wakati akifungua mjadala kati ya wanahabari na wataalam wa uhifadhi, kuhusu changamoto ya viumbe vamizi na ushiriki wa Serikali katika kudhibiti migogoro kati ya wanyamapori na wanadamu.

"JET inalenga kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi katika uhifadhi bainowai, ndiyo maana tunafundisha kuhusu sera, kupitia kwenu wanahabari tunajenga uwezo kwa wananchi, lakini pia watunga sera.

Ni muhimu wadau na Serikali kushirikiana kudhibiti migogoro kati ya wanadamu na wanyamapori, lakini pia changamoto ya viumbe vamizi kwenye uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii," amesema Dk. Otaru.

Katika mjadala huo viumbe vamizi wametajwa kuwa ni changamoto inayokua na kuleta athari kwa jamii, kiuchumi na uhifadhi bainuwai hivyo kuzorotesha ustawi wa maendeleo ya taifa.

Akitoa mada katika mjadala huo, Mtaalam wa Uhifadhi Bainuwai kutoka Mradi wa USADTuhifadhi Mazingira, Joseph Olila amesema jitihada zaidi zinahitajika kukabili changamoto ya viumbe vamizi iliyoenea maeneo mbalimbali nchini na kwamba udhibiti wa changamoto hiyo ni gharama kubwa, hivyo kunahitaji ushirikiano wa nyanja zote.

"Viumbe vamizi ni wasio wa asili, inaweza kuwa mmea, wanyama au wadudu. Huota au kuletwa kutoka eneo jingine na kuleta madhara kwenye mazingira, uchumi au jamii," amesema Olila.

Akifafanua, Olila amesema: "Viumbe vamizi vinaharibu mfumo wa utalii, watu wanaweza kuacha kutembelea vivutio kwani vile vya asili hupotea au kuharibika. Huondoa viumbe vya asili na kuvuruga pia mfumo wa chakula kwa viumbe hivyo, kupoteza bainoai ya asili, kueneza magonjwa kwa mimea na wanyama, hata kuharibu miundombinu ya mabwawa na maziwa."

Kwa mujibu wa Olila viumbe hivyo pia huvuruga maisha ya kitamaduni, kuwa tishio kwa afya za watu kwa kusambaza magonjwa au kusababisha mzio hata kufanya gharama za afya kuongezeka katka familia na taifa.

Kwa upande wake, Meneja Ufuatiliaji wa Mradi wa USAIDTuhifadhi Maliasili, John Noronha amesema mara nyingi migogoro kati wanyama na wanadamu hutokea wakati binadamu wanapoingia maeneo ya wanyamapori ambapo madhara hutokea, hivyo juhudi shirikishi za pamoja zinahitajika kwa Serikali na wadau wa uhifadhi kudhibiti hali hiyo, ikiwamo kuboreshwa kwa sera na sheria za uhifadhi maliasili pamoja na usimamizi wake.

Kuhusu kudhibiti viumbe vamizi amesema ni muhimu juhudi za makusudi zifanyike kuzuia visiingie katika mfumo wa uzalishaji, kuboresha sheria na kanuni za uhifadhi mazingira na kutoa elimu kwa jamii kuhusu changamoto hiyo na namna ya kuidhibiti.

 

No comments:

Post a Comment

Pages