HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 25, 2023

MSSTSP yanufaisha shule nne Dar

 

Na Selemani Msuya 


PROGRAM ya Kusaidia Kufundisha Masomo ya  Hisabati na Sayansi (MSSTSP) inayoratibiwa na Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi (CoNAS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika shule nne za Mkoa wa Dar es Salaam imewezesha kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Hayo yamesemwa na walimu wa shule nne za Manzese, Mugabe, Salma Kikwete na Yusuph Makamba wakati hafla ya kufunga MSSTSP awamu ya pili iliyonyika UDSM mwishoni mwa wiki ambapo walimu 16 wakujitolea walipatiwa vyeti.

 

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Manzese, Zubeda Kindamba amesema kupitia program hiyo wamefanikiwa kuongeza ufaulu kwenye masomo ya hisabati na sayansi ukilinganisha na miaka ya nyuma.


“MSSTSP imeleta ari ya wanafunzi kusoma masomo ya sayansi, kwani awali tulikuwa tuna mkondo mmoja, ila kwa sasa tuna mikondo mitatu na ufaulu umeongezeka. Lakini pia vijana hawa wakujitolea wametuongezea ujuzi na maarifa, hii program iwe endelevu,” alisema.



Zubeda ameomba UDSM kupitia CoNAS kuangalia uwezekano wa kuwaongezea wanafunzi, kwani shule yake ina zaidi ya wanafunzi 1,600, hivyo hitaji la walimu wa masomo ya sayansi ni kubwa.


Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Salma Kikwete, Ndevu Abasi amesema MSSTSP imewezesha wanafunzi nane kupata alama A kwenye somo la biolojia, A tatu kwenye Kemia na ufaulu umezidi kuongezeka.


“Walimu wangu ambao mmetulea sisi Salma Kikwete Sekondari wameleta mapinduzi makubwa kwenye masomo ya sayansi tunaomba mtuletee wengi zaidi,” amesema.


Makamu Mkuu Taaluma, Shule ya Sekondari Yusuph Makamba, Rahabu Nnko amesema program hiyo ni mwokozi kwao kwa kuwa awali walikuwa hawana mwalimu wa somo la fizikia, huku hesabu na kemia akiwa mmoja, ila kwa sasa wanafunzi wameongezeka kusoma masomo ya sayansi.



“Kidato cha nne wanaosoma mchepuo wa sayansi wapo 28 na cha tatu wapo 50, haya ni maendeleo makubwa kwetu, ila tumepata A za hisabati, biolojia, kemia na fizikia bado tunajikongoja,” alisema.


Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mugabe, Anna Chuka amesema shule yao ina wanafunzi zaidi 1,800 ila masomo ya sayansi hayana walimu, hivyo walimu wa MSSTSP wameweza kuwakomboa na kuomba kuendeleza program hiyo.


Nao Walimu wakujitolea Justin Justus wa Salma Kikwete na Tatu Maulidi wa Mugabe Sekondari wamesema program hiyo ni nzuri na inapaswa kuendelezwa, huku wakiomba Serikali iwape kipaumbele wakati wa kutoa ajira.

 

Awali akizungumza wakati wa akifunga program hiyo ya awamu ya pili, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utafiti UDSM, Profesa Nelson Boniface amesema chuo kinaahidi kuendeleza programu hiyo muhimu kwani inatekeleza malengo ya kuanzishwa kwa chuo hicho.


“Majukumu makuu ya UDSM ni kufundisha (kutoa maarifa), kufanya utafiti na kuchapisha matokeo ya tafiti hizo, pamoja na kutoa ushauri na huduma kwa jamii/umma, hivyo kuwezesha walimu 16 kwenda katika sekondari hizo ndio jamii hiyo,” amesema.

Rasi wa Ndaki ya CoNAS ambao ndio waratibu wa program hiyo, Profesa Flora Magige amesema MSSTSP imeongeza ubora wa ufundishaji na kuvutia wanafunzi kujishughulisha na masomo haya muhimu kwa ustawi wa Taifa.


Aidha, amesema walimu walioshiriki kwenye programu hiyo wamepata uzoefu mkubwa wa kazi ya ualimu kwani walipata fursa ya kushiriki katika shughuli za kiualimu zilizokuwa zikifanyika katika shule husika katika kipindi chote walichokuwa wanajitolea, mfano, kushika zamu, kutunga mitihani na kusahihisha.


 “Ndugu mgeni rasmi, pamoja na mafanikio makubwa, programu hii inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa fedha za kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa malengo ya uanzishwaji wake, kwani programu hii haina chanzo cha uhakika cha fedha,” amesema.

Mratibu wa Program Dk. Ally Mahadhy amesema kwa kipindi cha miaka miwili wamefanikiwa kupeleka walimu 32 katika shule hizo, ila malengo yao ni kuwafikia shule 25 katika mikoa mbalimbali. 

No comments:

Post a Comment

Pages