HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 04, 2023

Serikali yatumia bilioni 334 kununulia vifaa vya kufundishia

Serikali imetumia zaidi ya Shilingi milioni 334 kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, kujifunzia, vifaa saidizi na kujenga mabweni mawili pamoja na bima za afya kwa wanafunzi 122 wenye mahitaji maalumu.


Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akizindua usambazaji vifaa hivyo, mabweni  na utoaji wa bima za afya  kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kiwango cha juu na  magonjwa ya kudumu waliotoka katika familia zenye kipato duni.


Amesema vifaa hivyo vya kujifunzia na  saidizi vinakusudiwa kutatua changamoto kubwa ya uhaba wa vifaa katika vyuo vikuu ambapo itarahisisha ujifunzaji kwa wanafunzi wasioona, wenye ualbino, uoni hafifu, viziwi na wenye ulemavu wa viungo.


Ametaja vifaa vilivyogaiwa kuwa ni shimesikio 79 kwa ajili ya wanafunzi wenye uziwi, miwani ya macho 25, vioo kuza vinavyotumia umeme 25 kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu, Magongo 29 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo, masine za braille zinazotumia umeme 17, fimbo nyeupe 62, _orbit reader_ saba, karatasi za kuandikia maandishi ya braille box 124, kofia 43, _sun block lotion_ 600 na miwani za jua 27, kwa ajili ya wanafunzi wenye ualbino.



"Hizi zote ni juhudi za Rais  Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata elimu bila kikwazo niwaombe wazazi kutokuwaficha watoto hao," amesema Profesa Mkenda.


Mkenda almesema vifaa hivyo vitasambazwa katika Vyuo vikuu nane ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma ( UDOM), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM), Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam ( DUCE), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), 


Vingine ni Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Muhimbiki (MUHAS), Chuo Kikuu cha Ardhi ( ARU) na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).


Akizungumzia ujenzi wa mabweni mawili  katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko,  Prof. Mkenda amesema yatasaidia wanafunzi wenye ulemavu wa akili na usonji kukaa na kutulia shuleni kwa lengo la kujifunza kiufasaha.


Kuhusu BIMA za afya Waziri Mkenda amesema zitasaidia kuimarisha afya zao, mahudhurio kwa wanafunzi hao na kuongeza kiwango cha ufaulu.



Akimwakilisha  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo katika uzinduzi huo Naibu Katibu Mkuu Dkt. Frankilin Rwezimula amesema Wizara  katika mwaka wa fedha 2022/2023 imenunua vifaa vya kielimu na saidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma katika vyuo vikuu nchini vyenye thamani ya Sh milioni 182.6.


Pia amesema wizara hiyo imefanya ukarabati wa mabweni mawili, ujenzi wa jiko na ujenzi wa uzio kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji katika shule ya Msingi ya Uhuru mchanganyiko.


Naye Mkurugenzi wa Elimu Maalumu kutoka Wizara hiyo ya elimu , Dkt Magreth Matonya amesema Shule ya Uhuru Mchanganyiko ni ya kwanza Tanzania kupokea watoto wasioona pamoja na watoto viziwi kutokuona na sasa imeanza kupokea watoto wenye ulemavu wa akili na usonji ndio maana wizara imejenga mabweni ili kuwawezesha wanafunzi hao kusoma kwa utulivu.


Dkt. Matonya ametaja idadi ya wanafunzi  wenye ulemavu waliopo katika ngazi mbalimbali za elimu kuwa ni  wanafunzi 5545 elimu ya awali,  60,828 elimu ya msingi, 10,202 elimu ya sekondari, 128 wanachuo waliopo VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, 288 Vyuo vya ualimu  na 632 vyuo vikuu nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages