HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 06, 2023

TRA; KASI YA ULIPAJI KODI IMEONGEZEKA KWA KIWANGO KIKUBWA

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanznia (TRA), Richard Kayombo, akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo yaliyoandaliwa na mamlaka hiyo kwa waandishi wa habari ambao ni wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC). (Picha na Francis Dande).


 Afisa Mwandamizi Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Julieth Kidemi, akitoa mada katika semina hiyo.

 Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hamad Mterry akijibu maswali ya waandishi wa habari.

Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mafunzo hayo. Kushoto ni mwandishi mwandamizi Iche Mang'enya.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), Tausi Mbowe (kulia) akiwa na baadhi ya wajumbe wa DCPC wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa katika semina hiyo.

 

Leyla Mpinga

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kasi ya ulipaji kodi imeongezeka kwa kiwango kikubwa hali ambayo inaonesha kuwa watafanikiwa kufikia lengo lao la kukusanya shilingi trilioni 23.1 kwa mwaka wa fedha 2022/23.                             

Aidha TRA imesema uanzishwaji wa matumizi ya mfumo wa kidigitali umeweza kuondoa vishoka katika mamlaka hiyo na kupunguza foleni.  


                                
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanznia (TRA), Richard Kayombo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao ni wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Dar es Salaam (DCPC), walioshiriki mafunzo ya siku moja yaliyoandaliwa na mamlaka hiyo.        
    
Alisema kupitia mafunzo hayo jamii itaweza kupata elimu sahihi kuhusu faida za kulipa kodi, hali ambayo inawasaidia TRA kukusanya mapato kwa uhakika na wakati, alisema kodi ambazo zinalipwa zimekuwa zikitumika kwa maendeleo.                      

"Mwaka wa fedha 2022/23 tunatarajia kukusanya shilingi trilioni 23.1 na tunaona lengo linaenda kutimia, Juni 30 tutaweka taarifa rasmi ya ukusanyaji wetu, mambo yatakuwa mazuri," alisema.          

Kayombo alisema ufanikishaji wa lengo hilo unaendana na ufunguaji wa ofisi nyingi kwenye wilaya na mikoa, hivyo kusaidia wananchi kupata huduma karibu na maeneo yao. 

                   
"Mfano hapa Dar es Salaam wilaya tumezipa mamlaka ya kimkoa na tumefungua ofisi zingine kama Mbezi, Shekilango, Mbagala na kwingineko, hivyo tunaenda vizuri,"alisema.
          
Mkurugenzi alisema mfumo wa kigitali  umeongeza mwamko kwa wananchi kulipa kodi na kukata  mzizi wa vishoka ambao walikuwa wanasumbua walipa kodi,                  pia imesaidia kupunguza
 gharama kwa mlipa kodi kwenda ofisini na kuacha biashara yake.             
Kayombo alisema TRA inaendelea na maboresho ya mfumo huo wa kidigitali ili uweze kuwa na tija zaidi kwa mlipa kodi na nchi.          
                      
Akijibu swali kuhusu uwezekano wa kuunda jeshi la TRA kukabiliana na bidhaa zinazopita kwa njia ya magendo alisema kwasasa mamlaka hiyo inashirikiana na vyombo vingine kukabiliana na hali hiyo.                      

Kayombo alisema nchi ya Tanzania inapakana na nchi nane hivyo kupitia Idara ya Forodha TRA watahakikisha changamoto hiyo ya magendo inakabiliwa.       

"Mfano eneo la bahari tuna zaidi ya kilomita 1,400 kuna vipenyo vingi, hivyo njia ya kukabiliana na hii changamoto ni kushirikiana na wadau wote, kwani madhara ya magendo sio kukwepa kodi pekee, bali unaweza kuhatarisha afya za wananchi kwa kuingiza bidhaa zenye madhara,"alisema.            

Mkurugenzi huyo alisema mipango na mikakati ya TRA kuongeza mapato na kukabiliana na wakwepa kodi ni kwa waandishi wa habari kutumia kalamu zao kizalendo kuelimisha jamii faida na hasara.

No comments:

Post a Comment

Pages