HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 03, 2023

Ustadh Rajabu abomoa ngome ya upinzani Tanga



Mwenyekiti wa shina la barabara ya 18 akimsomea taarifa Mwenyekiti wa mkoa.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Ustadh Rajab mara baada ya kufungua kijiwe cha vijana wa Madina.


Na Mashaka Mhando, Tanga


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi CCM mkoani Tanga, Ustadh Rajabu Abdalahman Abdalah MNEC, amekomba vijiwe vya Chama cha ACT- Wazalendo na CUF vilivyokuwa nguzo ya vyama hivyo katika Jiji la Tanga, tangu kuanza mfumo wa vyama vingi 1994.


Vijiwe hivyo, vilivyopo kata ya Ngamiani Kusini, vilikuwa ngome ya upinzani kuanzia Chama Cha Wananchi (CUF) na baadae ACT-Wazalendo ambako kinara wa chama hicho Abdulhaman Hassain Omari tayari amejiunga na CCM pamoja na wanachama wengine.


Wakizungumza mara baada ya Mwenyekiti kufungua mashina na vijiwe hivyo, vijana walimweleza Mwenyekiti kuhusu mikopo ili waweze kuongeza mitaji yao na kufanya biashara za uhakika.


"Mheshimiwa Mwenyekiti moja ya changamoto zinazotupata ni kukosa mitaji, mikopo inayotolewa na halmashauri ni kazi kutufikia," alisema Salmini Ganga Mwenyekiti wa shina lililopo barabara ya 18  na wanachama 50 kati ya hao 30 kutoka upinzani.


Alisema vijana wengi wanajishughulisha na bodaboda lakini pia wakipata gunia mbili za viazi wanaweza kuanza biashara ya chips ili wapate mahitaji na familia zao. Mwenyekiti aliitisha harambee ikapatikana sh. 270,000 akawapa vijana hao.


Akizungumza katika vijiwe hivyo, Mwenyekiti alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anafanya maboresho ya mikopo ya asilimia 10  inayotolewa na halmashauri ili iweze kuwasaidia wananchi kuliko mfumo wa sasa.


"Ndugu zangu zile asilimia 10 zinazotolewa na halmashauri 4 vijana, 4 wanawake na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu, Rais anzifanyia maboresho ili ikianza kutolewa ilete tija kwa watu wanaokopeshwa" Alisema na kuongeza,


" Awali ilikuwa wengi hampati, sasa Rais amekuja na maboresho ili zikitolewa ziweze kuwanufaisha katika shughuli mnazofanya,".


Alitoa mfano kundi la watu watano wakipewa milioni tano ilikuwa haiwasaidii kuinua maisha yao.


Mwenyekiti huyo alisema pamoja na maboresho hayo ya mikopo, fedha kiasi cha shilingi bilioni 429 zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha bandari ya Tanga ambazo zitasaidia uchumi na ajira kwa vijana.


Aliendelea kusisitiza wananchi wa mkoa wa Tanga kumuunga mkono Rais Dkt Samia kutokana na kuifungua nchi kwa miradi mbalimbali ya kimkakati kwa nchi ikiwa ni pamoja na kuboresha sekta za elimu, afya, maji na miundombinu.

No comments:

Post a Comment

Pages