HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 20, 2023

Mbunge wa Ukonga aja na Nane Nane Cup

 NA JOHN MARWA

 

MBUNGE wa Jimbo la Ukonga, jijini Dar es Salaam Jerry Silaa, amesema  Bonanza la michezo la Jerry Silaa Cup ‘Nane Nane Cup’ kwa wananchi wa jimbo hilo linaenda kutoa burudani ya haja kwa vijana na wazee.

 


Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo jijini Dar es Salaam wakati wa kuzindua na kuelezea dhima na muelekeo wa Bonanza hilo amesema ni sehemu ya kuwakutanisha pamoja, kujenga afya na kuendeleza vipaji kwa vijana.  

 

“Jimbo la Ukonga ni jimbo kubwa wote mnafahamu na  Mbunge ni mpenzi wa michezo na wako vijana wengi wanaofanya shughuli za michezo, mpira wa miguu, rede, chandimu na michezo mingine. Tumekuwa tukifanya mabonanza vipande vipande leo msongora, mara tuko kivule , gongo la mboto na safari hii tumekuja tofauti.

 

“Tumekuja tofauti kwa kuandaa bonanza kubwa la ‘Nane Nane’ ambalo litatanguliwa na michezo ya mitoano ya timu za Veterani, tuna timu 16 za Veterani kwenye jimbo letu la Ukonga lakini vilevile tuna timu 114 za vijana za kawaida timu za mitaani ambazo zote ukisema zicheze pamoja huwezi kumtoa leo mtu kitunda aende mpaka Chanika gharama inakuwa ni kubwa. 

 

“Kwaiyo tutakuwa na vituo mbalimbali, watu wa Kitunda, Kivule Mzinga watacheza pamoja kwenye maeneo yao, tutakuwa na kituo cha Ukonga na Gongo la Mboto, tutakuwa na kituo cha watu wa Pugu na maeneo yanayozunguka, tutakuwa na kituo cha Chanika, Msongola wacheze vijana wenyewe.” Amesema Silaa na kubainisha kuwa.

 

“Lakini tutahitimisha pamoja siku ya ‘Nane Nane’ kwa kuwa na Bonanza kubwa ambalo litakuja kufanyika fainali za yale makombe madogo madogo  ya kila eneo pamoja na zile timu za Veterani ambazo zitakuwa zimeingia fainali kuja kumalizia pale lakini pia michezo ya lede haijaachwa nyuma ina ligi yake, mchezo wa chandimu nao haujaachwa nyuma una ligi yake lakini yote hitimisho lake itakuwa ‘Nane Nane’ pale viwanja vya ‘Nguvu Kazi’ Chanika.

 

“Nguvu kazi Chanika ndio senta na ni eneo ambalo lina viwanja vingi, kwaiyo ni viwanja ambavyo vinaweza vikachezesha wakati mechi za vijana zinachezwa uwanja A, uwanja B mechi za Veterani, lakini tutakuwa na burudani mbalimbali kwa maana ya kuweka pamoja wananchi wa jimbo la ukonga kuweza kujadiliana maswala mbalimbali ya maendeleo.

 

“Zipo kazi kubwa zinafanyika na Serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan, ujenzi wa madarasa ya Uviko, ujenzi wa madarasa ya pochi la mama, mradi mkubwa wa mwendo kasi awamu ya tatu Gongo la Mboto – Kariakoo, miradi midogo midogo ya barabara ndani ya Jimbo. Miradi mikubwa ya maji. Afya, vituo vya afya vingi vimejengwa, Zingiziwa, Majohe na Kipunguni na bajeti hii vituo vingine vitajengwa.” Silaa ameongeza kuwa.

 

“Kwaiyo tutatumia siku hii kucheza na kutaarifiana kwa sababu michezo ndio inakutanisha watu kwa pamoja, michezo ni afya, michezo ni ajira, kwaiyo tunategemea  kuwa na zawadi mbalimbali, kuna zawadi za Ng’ombe, kuna zawadi za Vikombe lakini ambacho kikubwa sana tutahakikisha kila timu itakayoshiriki itapata seti ya jezi kwa kushiriki tu. Afu watacheza sasa kwa maana ya kukuza vipaji na kuwania zawadi mbalimbali, zipo ligi ndogo zenye kombe la Mbuzi, zipo ligi kubwa zenye kombe la Ng’ombe na Vikobe.

 

“Yote ni katika kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Ukonga wanapata Burudani, vijana wa Jimbo la ukonga wanacheza na wazee wenzangu wa Veterani na wenyewe wanapata eneo la kuweka afya zao sawa kuepuka magonjwa na kujenga afya zao kwa ajili ya kujiweka fiti.”

 

Bonanza hilo linatarajiwa kuanza Julai 23 na kufika tamati Agosti 8 mwaka huu kwa zaidi ya timu 130 kumenyanyana kuwani, Ng;ombe, Mbuzi, Jezi na Vikombe.

No comments:

Post a Comment

Pages