Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, akizungumza wakati ya uzinduzi wa Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendele kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuhakikisha kuwa Vyuo na Taasisi za elimu ya Juu nchini, vinaimarisha ushirikiano na Taasisi za Utafiti na Sekta Binafsi, ili kuweka utaratibu wa kuendeleza teknolojia zinazoanzishwa nchini, na kuhamasisha matumizi yake ili kukuza na kuimarisha na kukuza kiuchumi katika jamii.
Profesa Mkenda ameyasema hayo Julai 18, 2023 katika Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, yenye kaulimbiu isemayo, Kukuza ujuzi nchini kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa uchumi imara na shindani
Amesema kuwa wakati umefika kwa TCU kuhakikisha inasimamia tafiti na kutoa ushauri kwa vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu kote nchini. ili kuweza kutoa majibu ya changamoto zinazoikabili jamii kwa kuhamasisha matumizi ya Teknolojia itakayochochea maendeleo katika jamii.
Aidha amesema kuwa Serikali imeendelea kutenga fedha kwaajili ya mikopo ya Elimu ya Juu, na kuendelea kufanya maboresho makubwa ya elimu ili kuhakikisha kuwa kila mtanzania mwenye sifa anapata fursa ya kufikia malengo yake kielimu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Profesa Penina Mhando amesema Serikali ipo kwenye mabadiliko ya mitaala na kwamba, TCU itaendelea kuchagiza Vyuo Vikuu kupokea mabadiliko hayo ili kuhakikisha vinaendelea kutoa elimu yenye ubora.
Maonesho hayo yameshirikisha Vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu zaidi ya 80 ambapo, yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi Julai 22, Mwaka huu.
No comments:
Post a Comment