HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 19, 2023

Vyama Vipya 18 vya Siasa vyaomba Usajil

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema kuna vyama vipya 18 vya siasa vimeomba usajili ambapo utaanza kutekelezwa baada ya kuhitimishwa zoezi la uhakiki wa vyama vilivyopo.



Shughuli ya uhakiki huo inatarajiwa kuanzia Julai 20 mwaka huu ambapo Ofisi ya Msajili kama mlezi inawajibika kulinda uhai wa vyama hivyo kwa kuvikagua na kubainisha mapungufu yanayojitokeza kisha kutoa muda kwa utekelezaji.


Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kikao kazi na viongozi wa Vyama vya Siasa nchini ikiwa ni maandalizi ya kuelekea kwenye uhakiki huo, Jaji Mutungi ameweka msimamo wake kwamba hawezi kuingia kwenye kusajili vyama vipya kabla ya kufanyika uhakiki katika vyama vilivyopo.


"Ni kweli kuna vyama 18 vimeomba usajili lakini siwezi kuendelea na mchakato kabla ya kufanyika uhakiki wa vyama vilivyopo, na kikubwa wawe na subra zoezi la uhakiki linaanza Julai 20 Mwaka huu tukimaliza nafikiri tunaweza kuendelea na mchakato," amesema.


Jaji Mutungi ameviambia vyombo vya habari kuwa shabaha ya kufanya mkutano wa leo unalenga kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo kuelekea kwenye uhakiki huo ili wasisumbuane na kuonekana kama ofisi hiyo imekuwa polisi.


"Tunahitaji tupeane uelewa wa kutosha ndiyo maana nimewakusanya wataalamu mbalimbali ikiwemo watendaji wa Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG)," amesema Jaji Mutungi.


Pia Jaji Mutungi amesema wanaotaka kufuta hati chafu ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa kuhakikisha vyama vinakuwa na wataalamu wa fedha ambao watakuwa wanafanya shughuli kwa kuzingatia weledi.


Nae, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameipongeza ofisi hiyo kwa kuandaa mkutano huo ambao kimsingi utasaidia kutoa uelewa na namna ya kuendesha vyama vyao kama viongozi.


No comments:

Post a Comment

Pages