Na Lydia Lugakila, Bukoba
Serikali mkoani Kagera imesema iko tayari kutoa kila aina ya uungaji mkono kwa vijana wa mkoa huo kuufanya mchezo wa masumbwi kupaa kitaifa na kimataifa.
Akizungumza wakati wa kufungua mashindano ya ngumi yaliyowakutanisha mabondia kutoka Mkoa wa Kagera na Mwanza Afisa Elimu Mkoa wa Kagera, Khalifa Shemahonge kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo amesema kuwa kutokana na Mkoa huo kuwa na historia ya michezo tangu kipindi cha nyuma na kufanikiwa kutoa wachezaji bora wa mpira ikiwemo timu ya Kagera Sugar na michezo mingineyo ni wakati sasa kuwaunga mkono Mabondia.
"Sisi kama Serikali tutahakikisha tunawapa ushirikiano na motisha katika mchezo wa Ngumi kwa maana hata Rais Samia ni mpenzi mkubwa wa michezo na michezo ameipa joto na kuwa mstari wa mbele kwa timu za taifa zilizoshiriki mashindano ya Kimataifa" amesema Khalifa Shemahonge.
Shemahonge amesema kuwa kutokana na Rais Samia kuwa mstari wa mbele usiku na mchana ili kuunga mkono suala la michezo kwa lengo la kuleta mafanikio makubwa na kulitangaza taifa la Tanzania ndivyo ambavyo Mkoa huo umejipanga kuunga mkono Vijana hao.
Mashindano hayo ya ngumi yaliandaliwa na Taasisi ya Zaa gwaaa boxing club chini ya Chama cha ngumi Mkoani humo muandaaji akiwa ni Mkurugenzi wa Zaa Gwaaa Wallace Rugangira Mkurugenzi wa Zaa Gwaaa lengo likiwa ni kuedeleza na kukuza mchezo wa ngumi shindano lililofanyika katika Uwanja wa Mashujaa uliopo Manispaa ya Bukoba.
Naye Mratibu Mkuu wa Pambano la Zaa Gwaaa Boxing Club Robert Kyaruzi ambaye pia ni Mwalimu wa wana Ndondi hao amesema ngumi si ugomvi hivyo WanaKagera wategemee makubwa kwani Vijana wataongezewa ujuzi ili kupambana zaidi kupitia Mkurugenzi wa Zaa Gwaaa ambaye ataendelea kupambania ngumi za Bukoba ziwe hai na kuongeza kuwa ushirikiano wa Viongozi ndio utaufanya mchezo huo kupaa katika anga za juu.
Aidha nao baadhi ya mabondia hao akiwemo Miraja Athuman kutoka mkoani Kagera na Mberwa Amosi wamewashukuru waandaaji wa shindano hilo na kuwa ili mchezo huo ukue na kuwatambulisha kitaifa na kimataifa Viongozi wa Ngumi wanatakiwa kuhamasisha mchezo huo pamoja na kufanya matamasha ya mara kwa mara ili kuwajengea uzoefu.
Hata hivyo nao mabondia kutoka Mwanza akiwemo Mbarook Bandwa na Anoel Seti wameipongeza Serikali mkoani Kagera kuwaleta pamoja kuonyesha vipaji vyao kwani tukio kama hilo la mchezo wa kirafiki kwa Mwanza halikuwahi kufanyika.
No comments:
Post a Comment