HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 17, 2023

Benki za NMB, NBC zatoa mkopo wa shilingi bilioni 470 kupiga jeki utekelezaji wa miradi ya maendeleo Visiwani Zanzibar

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akishuhudia  Utiaji wa Saini mkopo wa pamoja wa dola milioni 200 ( TZS biliioni 470) kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo visiwani Zanzibar  kati ya Benki ya NMB, Benki ya NBC  Pamoja na Wizara ya  Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar (kulia ), Katibu Mkuu Wizara ya Wizara ya  Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Akil akisaini kwa niaba ya Wizara  na Bw. Juma Kimori Afisa Mkuu WA Fedha NMB akisaini kwa niaba ya NMB. Hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar 


Benki za NMB na NBC zimeandika historia mpya visiwani Zanzibar baada ya kutoa mkopo wa pamoja wa dola za Marekani milioni 200 ( tarkiban shilingi bilioni 470) kwa lengo la kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo visiwani humo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.


Kupitia mkopo huu wa aina yake, Benki ya NBC ilichukua nafasi ya Mwekezaji Mkuu Aliyeidhinishwa yaani Mandated Lead Arranger (MLA) huku Benki ya NMB ikiwa mfadhili mwenza wa mkopo huo kwa Serikali ya Zanzibar ambao unatarajiwa  kulipwa ndani ya kipindi cha miaka 8.


Mkopo huo unalenga kufadhili huduma za kijamii na mipango ya maendeleo Visiwani Zanzibar ikiwemo miundombinu ambayo inalenga kuimarisha maisha, kukuza uchumi na kukuza maendeleo endelevu kwa jamii.


Akizungumza mara baada ya utiaji saini wa mikataba ya mkopo huo wakati wa hafla fupi iliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Afisa Mkuu wa Fedha WA Benki ya NMB Juma Kimori aliutaja mkopo huo kuwa wa kihistoria katika sekta ya benki na fedha nchini.


“Tuna heshima kubwa kuwa sehemu ya mkopo huu unaolenga kuunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ushiriki wetu katika mkopo huu unadhihirisha dhamira yetu ya dhati ya kusaidia maendeleo na ustawi wa jamii visiwani hapa Zanzibar,” Kimori alisema.


Kimori aliongeza, “Tunaamini mkopo huu utasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na kuchangia ukuaji wa maendeleo endelevu ya uchumi hivyo kuleta manufaa ya kudumu kwa wananchi wa hapa visiwani Zanzibar na kuchangia mustakabali wao wenye mafanikio.


Katika hafla hiyo alisisitiza dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuongeza kuwa benki hiyo mbali na kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo imekuwa na mchango mkubwa katika kuwekeza katika uwekezaji wa kijamii wa kijamii (CSIs) ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kukuza thamani ya wadau wake wote ikiwa ni pamoja na jamii ambako benki inafanyia kazi.


"Sisi kama benki, tutaendelea kuunga mkono kikamilifu utekelezaji wa Ajenda ya Uchumi wa Bluu ya Serikali ya Zanzibar kupitia utoaji wa huduma bora za kibenki ninazokidhi matakwa ya wateja wetu," alisema.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Theobald Sabi wakati wa hafla hiyo alieleza kufurahishwa na ushiriki wa benki yake katika mkopo huo akisisitiza kwamba utasaidia katika kufikia dira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya ukuaji wa uchumi jumuishi na upatikanaji wa maendeleo endelevu.


Sabi aliongeza kuwa mpangilio wa mikopo unaashiria mafanikio makubwa na utasaidia kufikia malengo ya pamoja ya uwezeshaji wa jamii, ushirikishwaji, na kusisitiza kuwa utaimarisha ustawi wa watu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar Saada Mkuya wakati wa hafla hiyo alisema fedha hizo zitasaidia kuboresha utoaji wa huduma za kijamii ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Maendelo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 2020/2026 inayolenga kuboresha miradi ya elimu, afya, miundombinu, maji na ujenzi wa viwanja vya michezo.


"Tulifanya mazungumzo na benki zoote za ndani katika harakati zetu za kupata vyanzo mbadala vya fedha na tunafurahi kwamba benki za NMB na NBC zilionyesha nia kuanzia mwanzoni. Tunafurahi kwamba leo tumesaini mikataba ya mkopo na benki hizi baada ya mazungumzo ambayo yamechukua karibu miezi na tunaamini huu ni mwanzo tu,” Dk. Mkuya alisema.


Naye  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi katika hafla hiyo alisema Serikali yake imepanga kutekeleza miradi ya maendeleo mara mbili mwaka huu ukilinganisha na miradi iliyotekelezwa mwaka jana kutokana na upatikanaji wa mkopo huu.


Alisema Serikali yake tayari imeweka mkakati kabambe wa kuhakikisha kuwa fedha za mkopo huo zinarejeshwa ndani ya kipindi cha miaka nane kama ilivyopangawa na kuwatoa hofu wote wenye wasiwasi juu ya Serikali yake katika suala zima la ulipaji wa mkopo huo.


“Leo tumeandika historia mpya kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kwa benki za ndani kutoa mkopo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya upatikanaji wa hizi fedha ambazo ni dola za marekani milioni 200, tumepanga kutekeleza miradi ya maendeleo mara mbili mwaka huu wa fedha ukilinganisha na mwaka jana,” Dkt. Mwinyi alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages