HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 08, 2023

SIKU YA OLIMPIKI YAFANA DAR

Na Tullo Chambo, RT

KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC), imeadhimisha Siku ya Olimpiki Duniani 'Olimpiki Day', Julai 8, kwa tamasha maalumu lililofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.



Siku ya Olimpiki duniani huadhamishwa na nchi wanachama kila mwaka Juni 23, ikiwa ni siku ambayo ilianzishwa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC), miaka 129 iliyopita.


IOC ilianzishwa Juni 23, 1894 jijini Paris Ufaransa, na hadi sasa ina wanachama 206 duniani kote, Tanzania ikiwamo.


Tamasha la leo jijini Dar es Salaam, lilipambwa na mbio za pole pole kwa watoto chini ya miaka 14  Kilomita 2.5 na watu wazima Kilomita 5, mchezo wa Teqball, Breaking na Skateboarding.


Washiriki kutoka sehemu mbali jijini Dar es Salaam na nje walishiriki, huku michezo ya Teqball, Breaking na Skateboarding ikiwa kivutio.


Akizungumza wakati wa tamasha hilo, Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi, alisema Tanzania imeamua kuadhimisha siku hiyo Julai 8 kutokana na Juni 23 siku hiyo kuadhimishwa barani Afrika huko Tunisia, ambako kulikuwa na michezo ya Afrika ya Ufukweni na viongozi wote wa kitaifa walikuwa huko.


Bayi, alisema tamasha la mwaka huu lilikuwa na ujumbe unaosema; 'Let's Move', na lengo lake ni kuihamasisha jamii kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya.


"Lengo la tamasha hili si kushindana, bali ni kuwajumuisha pamoja watu na kuwahamasisha kufanya mazoezi ili kujenga afya zao," alisema Bayi.


Aliongeza kuwa, lengo lilikuwa kushirikisha washiriki takribani 1000 na kuwapongeza waliojitokeza huku akitoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi mwakani wakati wa maadhimisho hayo.


Naye kijana mdogo Meshack Gotini mkazi wa Nyambwela Manispaa ya Temeke na mwanafunzi wa shule ya msingi Barabara ya Mwinyi, alielezea furaha yake kushiriki tamasha hilo na kueleza lina manufaa kwao.


"Kwanza michezo ni afya, sisi tunaposhiriki michezo hutufanya pia tuchangamke kiakili na kutusaidia hata katika masomo yetu, lakini pia ninapokuja hapa siondoki hivi hivi tu, tunapata fursa pia ya kukutana na wenzetu na kujenga urafiki pia," alisema Meshack.


Aidha katika tamasha hilo, washiriki wenye umri mkubwa na mdogi kuliko wote walitambuliwa na kuzawadiwa zawadi ya fedha taslimu.


Pia, washiriki wote walikabidhiwa vyeti vya ushiriki kwa kutambua ushiriki wao.

No comments:

Post a Comment

Pages