Baadhi ya wakulima wa zao la ufuta wakiwa kwenye mnada.
Na Khadija Kalili
SERIKALI Imefikisha Tani 700 za viuatilifu aina ya Salfa kwenye Chama Kikuu Cha Wakulima Mkoa wa Pwani CORECU kwa ajili ya zoezi la usambazaji kwa wakulima wa zao la korosho linaloendelea Mkoani humo.
Akizungumza na baadhi ya wakulima wa Mkoa huo kwenye mnada wa saba wa ufuta uliofanyika katika ghala kuu la Wilaya ya Kibiti Meneja wa CORECU Mantawela Hamisi amesema
maandalizi ya msimu wa zao la korosho kwa mwaka 2023 yameanza ambapo wakulima wameshaanza kupokea na kuanza kupulizia mikorosho yao viuatilifu vyao aina ya Salfa ya unga na ya maji.
Amesema matarajio waliyonayo ni kuwa Mkoa mzima wa Pwani kupitia Bodi ya Korosho Tanzania CBT na Chama hicho kikuu ni kupokea tani 1,000 ambazo zinaendelea kugaiwa kwa wakulima kiwilaya na Kata kulingana na Wakulima walivyojiorodhesha kwenye mfumo kupitia Maafisa Kilimo wao.
Amesema Tani 300 zingine bado hazijafika hivyo amewaomba wakulima kuwa wavumilivu na kusubiri kiasi hicho cha Salfa ambayo bado haijafika.
"Pindizitakapofika zinapokelewa kwenye mfumo ndipo watu wa Bodi ya Korosho Tanzania wanazichakata na kutoa maelekezo ya jinsi ya kugawana Salfa hiyo kulingana na mfumo unavyopanga"
"Yaani kadri Salfa zinavyoingia, ndivyo zinavyoingizwa kwenye mfumo na jinsi mfumo unavyogawa ndipo na sisi CORECU ndivyo tunavyowaletea Wakulima pembejeo zenu" amesema Hamisi.
Amesema usambazaji wa pembejeo hizo unaendelea katika Mkoa mzima wa Pwani na ameonesha magariaina ya malori yakipakia pembejeo hizo kuzipeleka katika Wilaya za Kisarawe, Mkuranga, Bagamoyo, Kibaha, Kibiti na Rufiji.
Meneja huyo ameonesha kushangazwa na mutikio mdogo wa wakulima kujisajili katika mfumo wa pembejeo kutoka katika Wilaya za Kibiti na Rufiji ambao ndiyo wamekuwa wakulima wakubwa wa mazao ya ufuta na Korosho na kujisababishia kupata mgao mdogo wa pembejeo hizo tofauti na Wilaya ya Mkuranga ambayo Wakulima wake wamejisajili kwa wingi hivyo wengi watapata pembejeo kuliko Wilaya zote za Mkoa wa Pwani.
"Mkuranga wameitikia zaidi kuliko Kibiti na Rufiji ambapo Wilaya ya Kibiti kuna Wakulima wengi zaidi,hivyo msijemkashangaa usambazaji wa pembejeo Wilaya ya Mkuranga ikawa imepokea pembejeo nyingi kuliko Wilaya ya Kibiti kwasababu wenzetu wameitikia kujisajili lakini huku sijui mlikuwa mnakwama wapi ?"
"Sasa madhara yake utasikia watu wana namba lakini hamjapata pembejeo ni kwakuwa hamkujisajili kwa wakati na muda umeshakwenda hivyo ninyi mliokuwa mkijivuta vuta ntakuja kupewa baadaye sana na endapo zikiisha tusijetukalaumiana"
Aidha Hamisi amesema pembejeo hizo serikali inazigawa kwa ruzuku ambapo mkulima hachangii kiasi chochote cha fedha lakini hazitatosheleza kila mkulima.
"Pembejeo hizo hazitatosheleza kila mkulima kwasababu pembejeo huletwa kwa namna mkulima alivyojisajili kwenye mfumo wa pembejeo".
"Mfuko mmoja wa Salfa utapulizia kwenye miti mia ya mikorosho sasa kama wewe una miche mingi kuliko pembejeo ulizopewa maana yake ni kwamba pale serikali ilipoishia kukusambazia unaruhusiwa kwenda kujitafutia sehemu nyingine kwa sababu serikali haiwezi kumuhudumia mkulima kwa mahitaji yake yote"
Pia amewataka Maofisa Kilimo waliohusika katika kusajili wakulima kwenye mfumo huo kwa kushirikiana na uongozi wa AMCOS za Kata husika wahakikishe wakulima wao wanapata pembejeo zao kama walivyojiandikisha.
Amesema bei ya ufuta iliyopitishwa katika mnada huo kuwa ni shilingi 3,805.34 kwa kilo moja.
No comments:
Post a Comment