HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 23, 2023

UDOM chawakaribisha Wanafunzi kujiunga Mwaka wa Masomo 2023/24 Wajengewe Uwezo na Maarifa ya Kujiajiri

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewakaribisha wahitimu wa Kidato cha Sita kutembelea banda la chuo hicho ili waweze kujionea kozi za fani mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo na kufanya udahili kwa mwaka wa masomo 2023/24.

Aidha, chuo hicho kimewasisitiza wahitimu hao kuchangamkia fursa za masomo yanayofundishwa UDOM kwani watakapojiunga watajengewa maarifa ya kuweza kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao.

Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Lughano Kusiluka katika Ufunguzi wa Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa wanafunzi watakaojiunga na UDOM watapata fursa ya kufundishwa fani mbalimbali kwa umahiri ili kuwajengea hali ya kujiamini pale wanapohitimu wawe na mawazo na uwezo wa kujiajiri.

" Tumekuja hapa kwa ajili ya kuwaelimisha wanaotaka kujiunga UDOM nawakaribisha wanafunzi waje kusoma katika chuo hiki kwani watapata elimu bora itakayowajengea uwezo wa kufikiria kujiajiri," amesema Profesa Kusiluka.

Amebainisha kuwa chuo hicho ni kikubwa na kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 32,000 na kwamba kimejengwa mahasusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa Watanzania wengi hivyo wanafunzi wacahangamkie fursa za masomo chuoni hapo.

Amesisitiza kuwa UDOM kinatoa zaidi ya Progamu 80 katika Ngazi ya Shahda ya Awali na progarmu zaidi ya 56 kwa ngazi ya Shahada za Umahili huku akibainisha fani zinazotolewa ni Udaktari, Uchumi, Sheria, Sosholojia, Utawala wa Biashara, Biashara na Uhasibu, Biashara katika Rasilimali Watu, Ujasiriamali na Biashara ya Kimataifa.

Nyingine ni Utalii, Masoko, Mazingira, Takwimu, Ununuzi  na Ugavi, Teknolojia ya Habari na Mwasiliano (TEHAMA), Jiolojia, Kemia, Madini, Petroli, Nishati Mbadala, Elimu, Lugha, Uhusiano wa Kimataifa, Ikolojia, Uandishi wa Habari na Mahusiano ya Umma na Fizikia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa UDOM, Rose Joseph amewakaribisha wanafunzi kujiunga na chuo hicho kwani kina mazingira rafiki ya kujisomea watapokuwa chuoni hapo.

Maonesho hayo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo Kukuza Ujuzi nchini Kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na Uchumi Imara na Shindani huku yakishirikisha Vyuo Vikuu na Taasisi ya Elimu ya Juu zaidi ya 80 yakitarajiwa kuhitimishwa Julai 22 mwaka huu.


   

No comments:

Post a Comment

Pages