HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 17, 2023

Uhakiki wa vyama vya siasa Julai 23, 18 vyaomba usajili

Na Selemani Msuya


OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imesema  kuanzia Julai 23 mwaka huu itaanza uhakiki wa vyama vya siasa ambavyo vina usajili wa kudumu, huku vyama 18 vipya vikiomba usajili.


Hayo yamesemwa na Msajili wa Vyama hivyo, Jaji Francis Mutungi  wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua kikao kazi kati ya ofisi yake na viongozi wa vyama, kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Jaji Mutungi alisema ofisi yake ina jukumu la kisheria la kufanya uhakiki wa vyama vya siasa kila mwaka, hivyo ameona kabla hajaanza kufanya uhakiki huo, waanze kutoa elimu kwa viongozi kwanza.


Alisema lengo na madhumuni ya kukutana ni kuwaanda viongozi hao na uhakiki, ili ofisi ya msajili ikianza kazi ipate urahisi.


“Tunataka kuchukua lile jukumu la kuwa walezi wa vyama vya siasa na katika kufanikisha hilo ni lazima tufanye uhakiki, ili tukidhi matakwa ya sheria ambayo yanatutaka tuhakiki,” alisema.


Jaji Mutungi aliwataka viongozi wa vyama kutoa ushirikiano wakati wa uhakiki unapoanza, ili kurahisha zoezi ambalo lipo kisheria.


Mutungi alisema uhakiki uliopita walibaini mapungufu mengi ndani ya vyama ambayo yanarekebishika, ambapo walitoa maelekezo yakurekebisha na imani yake ni kuona mchakato ukianza watakuta mazingira mazuri.


Alisema katika uhakiki uliopita walibaini vyama vingi vimekutwa na hati chafu na zisizoridhisha, hivyo kupitia mafunzo hayo vyama vitaelewa umuhimu wa kujiendesha kama taasisi na sio mali ya mtu binafsi.


Jaji Mutungi alisema hapendezwi na taarifa za ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinazoonesha vyama kutofanya vizuri kuendelea.


Aidha Jaji Mutungi alisema hadi jana ofisi yake imepokea maombi 18 ya vyama vipya vya siasa na kwamba kwa sasa wanaendelea na mchakato wa usajili, hivyo wakimaliza zoezi la uhakiki ndipo waendelee na usajili.


Alisema ofisi itatoa usajili kwa chama chochote ambacho kitakidhi vigezo ila wameona wamalize zoezi la uhakiki ambalo lipo mbele yao.


“Sisi tunaendelea na zoezi la uhakiki wa vyama vyenye usajili wa kudumu, baada ya hapo tutaendelea na mchakato wa kusajili, kwani haingii akilini unasajili chama kipya, huku kukiwa na vyama ambavyo havikidhi vigezo na hujavihakiki,” alisema.


Kwa upande wake Mwenyekiti Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amesema wanachofanya ofisi ya msajili ni utekelezaji wa  Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo imetoa maelekezo kwa vyama kuhakikiwa kila mwaka, ili kuangalia vinavyojienesha.

“Huu uamuzi wa ofisi ya msajili kukutana na viongozi wa vyama ni wa kuungwa mkono na kila kiongozi wa chama cha siasa kwani unatukumbusha majukumu yetu kwa mujibu wa sheria, sisi CUF tunaupongeza na tunaahidi kushirikiana na ofisi hiyo,” alisema.


Lipumba alisema changamoto za vyama kupata hati chafu na zisizoridhisha zinatokana na ukweli baadhi ya viongozi katika ngazi ya chini kushindwa kutumia mifumo ya kisasa kwenye kutoa huduma, hivyo kukosekana ushahidi.


Mwenyekiti wa Chama Chama Cha Alliance for Democratic Change ( ADC), Hamad Rashid Mohamed alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa vyama vyote ili kuhakikisha changamoto za hati chafu zinaisha.


Alisema uchanguzi wao unaonesha kuwa vyama vya siasa vinapata hati chafu kutokana na kukosa elimu ya namna ya kutunza kumbukumbu za matumizi ya fedha, hivyo anaamini mafunzo hayo yaliyoandaliwa na ofisi ya msajili yataweza kuwakumbusha majukumu yao.


“Kuna vyama vinapata hati chafu kutokana na kukosa mfumo mzuri wa uongozi kuanzia chini, hivyo Serikali ina wajibu wa kuvisadia ili viweze kuimarika, lakini kuna vyama vimekuwa na mtandao hadi nje ya nchi, hilo nalo linatakiwa kuangaliwa kwa jicho la ziada ili kuepuka uwepo wa misaada yenye mashaka,” alisema.


Naibu Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara,  Anamringi Macha alisema  vyama vya siasa vipo kwa ajili ya kufanya kazi za maslahi ya Taifa, hivyo ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuvihakiki ni kuvifanya vikidhi matakwa ya kisheria.


Macha alisema CCM imekuwa ikizingatia sheria ya vyama vya siasa katika kutekeleza majukumu yake hali ambayo imesababisha kisiwe na hati chafu.
 Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Pages