Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, akitoa akifafanua jambo wakati wa mkutano wa Wahariri na Waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam Julai 17, 2023. (Picha na Francis Dande).
Mwanachama wa Jukwaa la wahariri (TEF) Angel akilimali, akizungumza katika mkutano huo.
Exuperius Kachenje
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimewahimiza watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji mbalimbali zinazoratibiwa na kituo hicho.
Akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TIC, Gilead Teri ametoa rai hiyo.
Amesema hatua hiyo itawawezesha watanzania kushiriki moja kwa moja katika ukuzaji wa uchumi wa taifa na kuzalisha ajira.
"Uwekezaji si ajira ni imani, tafsiri ya uwekezaji ni Mtaji,rasilimali na teknolojia. Uwekezaji ni nyenzo muhimu kwa taifa kuendelea na kukuza uchumi, tuwekeze kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo," amesema Teri.
Teri amesema kasi ya kukua kwa uwekezaji Tanzania ni kubwa na TIC ipo kwa ajili ya kuwasaidia wao kunufaika na mageuzi hayo, hivyo ni muhimu kwa watanzania kunufaika na fursa zinazotokana na mageuzi makubwa ya uchumi na teknolojia.
"Hata sasa, idadi ya wawekezaji wa ndani wanaosajiliwa ni kubwa kuliko wakati wowote. Tumesajili asilimia 49 wawekezaji wa ndani na asilimia 33 wa nje.Tunalenga kufikia asilimia 100,"amesema bosi huyo wa TIC.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, Tanzania ina mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki na SADC kutokana na gharama kuwa chini ikiwamo za umeme.
No comments:
Post a Comment