Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Waziri
wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewataka Wakala wa
Barabara nchini -TANROADS kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa
Mkandarasi atakayejenga Daraja la Mto Msimbazi ili kuwaondolea wakazi wa
Jiji la Dar es Salaam, changamoto ya mafuriko.
Dkt.
Nchemba ametoa kauli hiyo baada ya kuongoza Ujumbe wa Serikali na Benki
ya Dunia kutembelea eneo la Jangwani ambapo mradi wa uendelezaji wa
Bonde la Mto Msimbazi, unatarajiwa kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa daraja
kubwa la juu la Jangwani, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mapema mwakani,
kwa gharama ya zaidi ya dola za marekani milioni 350.
“Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ametuelekeza tufanye kikao na Benki ya Dunia ili mradi huu wa daraja na
ujenzi wa barabara za Jiji la Dar es Salaam, uanze kutekelezwa haraka
ili kuwaondolea wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kero ya mafuriko pamoja
na kuimarisha mipango miji” Alisema Dkt. Nchemba.
Alisema
kuwa Jiji la Dar es Salaam ni kitovu cha biashara na linategemewa na
nchi zaidi ya nane zinazopakana na Tanzania na kwamba kukamilika kwa
miradi hiyo ya daraja na barabara za Jiji hilo zitachochea shughuli za
kiuchumi.
“Wizara
ya Fedha kupitia Benki ya Dunia tunawahakikishia kuwa fedha zipo
kinachotakiwa ni kuanza kwa utekelezaji ili kutekeleza maelekezo ya Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”
Alisisitiza Dkt. Nchemba.
Naibu
Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Deo Ndejembi, ambao ndio
watekelezaji wa mradi huo, wameahidi kusimamia utekelezaji wa mradi huo
kwa ufanisi ili thamani ya fedha itakayotumika ilingane na ubora wa
mradi.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila,
alihimiza pia kuanza haraka kwa ujenzi wa mradi huo ili kutatua kero za
wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na kuzingatia usanifu wa viwango vya
juu.
“Ujenzi
wa barabara na madaraja makubwa kama haya kuna maanisha kuufungua mkoa
kiuchumi sasa tusibaki kulumbana na kubishana kwa ajenda ndogo ambazo
wakati fulani hazina mashiko kwa mustakabali wa Taifa letu, lakini pia
ile maana halisi ya Mkoa wa Dar es Salaam kuwa Jiji la kibiashara iweze
kuonekana kwa miundombinu hii” alisema Bw. Chalamila.
Naye
Mbunge wa Ilala Mussa Azzan Zungu, alisema kuwa Serikali inaboresha
Bandari ya Dar es Salaam kwa kumpata mwekezaji DP World ambapo mizigo
mingi itakayopokelewa, mizigo ambayo inahitaji barabara bora ili
kuharakisha uondoshaji na usafirishaji wa mizigo kwenye nchini na nchi
Jirani ambapo nchi inatarajia kupata zaidi ya shilingi trilioni 26 kwa
mwaka kutokana na uwekezaji huo, fedha ambazo zitachangia maendeleo ya
nchi.
“Kama
mnavyofahamu, Jiji la Dar es Salaam linachangia asilimia 85 ya pato la
Taifa na kwamba kukamilika kwa mradi huu kutachangia upatikanaji wa
fedha za kutosha kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya Taifa” alisema Mhe.
Zungu
Mwakilishi
Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete, alisema kuwa Benki yake
itatoa mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 350 ili miradi hiyo
itakayotekelezwa Jijini Dar es Salaam iweze kuchangia maendeleo ya nchi
kwa kupanga mji, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuboresha
miundombinu ya usafiri na kudhibiti taka ngumu.
Baadhi
ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamepongeza hatua ya Serikali ya
kuweka miundombinu imara ya jiji hilo itakayosaidia kuwaondolea kero ya
foleni na mafuriko wakati wa mvua zinaponyesha.
Walisema
kuwa wamekuwa wakipoteza muda na mali zao wakati wa mafuriko na kwamba
ujenzi wa daraja hilo kubwa na refu litakaloanzia Magomeni hadi Fire,
utakuwa mwarobaini wa matatizo yao na kummwagia sifa Mheshimiwa Rais
Samia Suluhu Hassan kwa kulivalia njuga suala hilo.
Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi (DMDP II) utatumia fedha hizo za Serikali na mkpo kutoka Benki ya Dunia kujenga miundombinu ya barabara, mifereji, maeneo ya wazi, masoko, vituo vya mabasi, na kurekebisha miundombinu ya taka ngumu, miundombinu ya usafiri, mabadiliko ya tabia nchi kwa jiji la Dar es Salaam zinazosababisha mafuriko na kudhibiti taka ngumu
No comments:
Post a Comment