HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 02, 2023

ROBERTINHO AMKABIDHI NGOMA SIMBA SC

Na John Marwa 


MARA tu baada ya kikosi cha Mnyama Simba SC kurejea wakitokea Uturuki, Kocha Mkuu, Roberto Oliviera (Robertinho) amesema atakuwa na wakati mgumu kupanga kikosi chake kutokana na wachezaji wake kuimarika zaidi.

Amesema uimara wa wachezaji wake umetokana na maandalizi mazuri yanayoendelea kufanyika na benchi lake la ufundi na kuwepo kwa wachezaji bora katika kila idara kikosini.


Baadhi ya nyota waliopo kwenye kikosi chake ni Clatous Chama,  Jean Baleke, Sadio Kanoute,  Saido Ntibazonkiza,  Kibu Denis, John Bocco. Mohammed Hussein na  Shomary Kapombe.


Mbali na hao wapya ni Luis Miquissone,  Willy Essomba Onana,  Kramo Aubin, Che Fondoh Malone, Fabrice Luamba Ngoma, wazawa ni Iddi Chilunda na David Kameta.


Simba waliweka kambi Uturuki kujiandaa na msimu mpya wa 2023/24 wa  mashindano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo katika maandalizi yao wamecheza mechi nne za kirafiki wakishinda mbili sare moja na kupoteza moja.


Akizungumzia na Habari Mseto Media mara baada ya kuwasili nchini, Robertinho amesema timu yake imesheheni wachezaji wazuri, wale waliokuwepo msimu uliopita na wapya ambao wote wamekuwa na uwiano mzuri katika viwango vyao.


Amesema wanaenda kuyatumia makundi mawili, kundi la kwanza liko daraja la juu likiwa na wachezaji bora zaidi kuliko msimu uliopita na kila mmoja akiwa na kiwango kizuri na kuonyesha ushindani mkubwa wa kuitaka jezi.


“Naipongeza klabu ya Simba, Rais wa Heshima, na watendaji wengine kwa kazi waliyoifanya, kwa sababu  sasa tuna uwiano mzuri wa kufanya mabadiliko ya wachezaji tunapopata majeruhi  kwenye kikosi cha kwanza ni jambo la muhimu sana kuwa na kikosi kipana,” alisema Robertinho.


Alibainisha kuwa watamuheshimu kila mpinzani watakae kutana naye lakini malengo yao ni  kutwaa mataji yaliyo mbele yao na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa. 


Robertinho ameeleza  kuvutiwa na uwezo wa nyota wapya kwenye Kikosi akiwemo Fabrice Ngoma ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wakiwa Uturuki, huku malengo yao kama timu ni kushinda Makombe.


Amesema anaamini kiwango cha kiungo huyo,  anataka kumuona akitumia kiwango chake kutoa mchango katika timu ili wafikie malengo yao msimu ujao kimataifa.


Ameongeza kuwa kiungo huyo ana CV kubwa ya kuzichezea klabu kubwa Afrika, ana uzoefu wa kucheza michuano mikubwa, anataka kumuona akitumia kipaji chake kuipa mafanikio Simba msimu ujao.


"Kwa kushirikiana na wachezaji wenzake, naamini ataifanyia mengi makubwa Simba huku akitoa nafasi ya kujiandaa zaidi kwa kuongeza mazoezi ya fitinesi ili awe fiti zaidi ya hapo.


"Ngoma ni kati ya wachezaji ninaowategemea kuelekea msimu ujao, nimempa kazi kubwa ya kuhakikisha anaipambania timu kutokana na uzoefu wake wa kucheza michuano mikubwa ya kimataifa," amesema Robertinho.



“Kwangu sina hofu  kabisa, katika mchezo wa kirafiki tuliocheza Ngoma alicheza katika kiwango kikubwa, lakini hajaonyesha ubora wake ambao ninaufahamu,” amesema Robertinho.


No comments:

Post a Comment

Pages