Na Irene Mark, Kibaha
WAKATI Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikitaraji kutoa utabiri wa Msimu wa Vuli leo Agosti 24,2023 imesema usahihi wa utabiri wa msimu wa masika umekwenda sawa kwa asilimia 86.4.
Akizungumza kwenye kikao kazi kati ya watumishi wa TMA na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali hapa nchini, iliyofanyika mjini Kibaha jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a, amesema usahihi wa taarifa hizo ni matokeo ya ufuatiliaji makini wa viashiria vya utabiri, wataalam na vitendea kazi vya kisasa.
Alisema Serikali imeendelea kuijengea uwezo TMA na kuifanya iendelee kuimnarisha huduma ikiwemo utoaji wa taarifa za hali ya hewa kila wakati na kuwafikia watumiaji ambao huzipata kwa usahihi na kufanya uamuzi.
Utabiri wa msimu wa Vuli unatarajiwa kuanza Oktoba, Novemba na kumalizika Desemba mwaka mwaka huu na kusisitiza kwamba ni msimu muhimu kwa wakulima kuandaa mashamba ili kufanya kilimo chenye tija kwa uchumi wa nchi.
"Kwa sababu hii tunawaomba waandishi wa habari mpeleke taarifa hizi sahihi kwa walengwa na watumiaji wa taarifa za hali ya hewa kwenye shughuli za maendeleo.
"Vuli ya mwaka huu kwa mujibu wa wataalam wetu ni tofauti na miaka mingine kwa kuwa inatarajiwa kuwepo na Elnino inayosababishwa na ongezeko la joto juu ya uso wa bahari kwa eneo la kitropiki la kati ya Bahari ya Pasifiki," alisema Dk. Chang'a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi.
Akizungumzia hali hiyo, Mtabiri wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Rose Senyagwa alisema athari za ongezeko la joto hilo husababisha kuongezeka kwa viwango vya mvua na joto kwa baadhi ya maeneo hapa nchini, hivyo kufanya msimu wa mvua kuwa ni miongoni mwa misimu muhimu ya kilimo hapa nchini hususani maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment