HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 24, 2023

TMA: Ni Vuli ya Elnino

Na Irene Mark

KAIMU Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a, amesema mifumo ya uchakataji wa taarifa za hali ya hewa inaonesha kuwepo kwa mvua za juu ya wastani hadi wastani wakati wa msimu wa vuli 2023 zitakazosababisha Elnino hafifu kwenye mikoa inayopata misimu miwili ya mvua.

Aliitaja mikoa hiyo ni Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba.

Maeneo mengine ni mikoa ya Mara, kaskazini mwa Mkoa wa Simiyu, Arusha, Manyara na Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua.

Akitoa utabiri huo mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Dk. Chang'a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), alisema   kutokana na uwepo wa Elnino, vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kuwepo Septemba, 2023 katika baadhi ya maeneo nchini, hata hivyo mvua za vuli, 2023 zinatarajiwa kuanza rasmi Oktoba, 2023 katika maeneo mengi ya nchi.

"Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Septemba, katika maeneo ya magharibi mwa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine ifikapo wiki ya pili ya Oktoba.

"Kwa kawaida mvua za vuli humalizika Disemba, hata hivyo msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea hadi Januari, 2024.

"Wataalam wetu wameona kuna ongezeko la mvua linatarajiwa kuwepo Desemba, 2023 ambapo tunaamini kipindi hicho Elnino inaweza kuongezeka," alisema Dk. Chang’a.

Dk. Chang’a alitoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za utabiri wa saa24, siku 10, mwezi na tahadhari zinazotolewa na TMA ikizingatiwa kuwa mwelekeo wa mvua uliotolewa ni kipindi cha miezi mitatu, hivyo viashairia vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadaliko ya muda mfupi utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Dk. Chang’a alisema, Mamlaka yake itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika.

Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.



No comments:

Post a Comment

Pages