Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF),
Joseph Butiku akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kongamano la BRI
linalofanyika nchini kuanzia kesho.
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, anarajiwa kufungua kongamano la kimataifa la kusherekea miaka 10 ya ushirikiano baina ya nchini za Afrika Mashariki na China litakalo fanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuanzia Agosti 25 hadi 26, 2023.
Ushirikiano wa China na Afrika Mashariki unatekelezwa kupitia Mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI) ambao una lengo la kuchochea amani, umoja na maendeleleo kwa nchi husika.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema katika kongamano hilo linatarajiwa kuwa na washiriki 180 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na China.
Alisema baada ya Naibu Spika Zungu kufungua kongamano hilo kutakuwa na uwasilishaji wa mada mbalimbali za kuelezea namna BRI ilivyofanya kazi kwa miaka 10 na namna ya kwenda mbele.
Mwenyekiti huyo alisema kongamano hilo la kimataifa limeandaliwa na MNF kwa kushirikiana na Ubalozi wa China, hivyo matumaini yake litaweza kukidhi hitaji la nchi husika.
Mwenyekiti huyo alisema China inatumia BRI kuhakikisha kila upande unanufaika, kwani historia inaonesha nchi hiyo imekuwa ikitekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa nchi husika.
Alitoa lea mfano Nchi ya Tanzania imenufaika kwa kushirikiana na China katika eneo la elimu, afya, kilimo, miundombinu aambapo alitaja mraji wa ujenzi wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), Jengo la Makao makuu ya MNF, Chuo cha Siasa Kibaha na Bunge la Tanzania.
“China miaka yote wamekuwa marafiki tukishirikiana kwa shida na raha katika masuala ya kilimo, nguo, viwanda, uzalishaji, ulinzi, miundombinu na hata kupigania uhuru,”alisema.
Alisema China imekuwa ikihitaji kuwepo kwa dunia yenye amani, umoja na maendeleo kwa watu wote na hilo limedhihirika kwao kwani hawajawahi kutamani utawala mwingine na wamekuwa wakifanya biashara zao kwa amani.
Butiku alisema anatamani kuiona dunia ikiendelea kuwa na amani na kuwepo shughuli za kiuchumi kwa maendeleo ya watu wake, kama China inavyofanya.
Alisema kongamano hilo ni ushahidi tosha kuwa China imedhamiria kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika Mashariki na kwamba matumaini yake ni kuona utekelezaji katika yale ambayo watakubakubaliana.
Mwenyekiti huyo alisema kongamano hilo litajadili mambo yanayoendelea kati ya Tanzania na China, mafanikio na changamoto walizozibaini ndani ya miaka hiyo na kupendekeza namna ya kupata ufumbufuzi.
Alisema katika miaka 10 ya kutekelezwa kwa mpango huo,katika mataifa mbalimbali duniani hususan Bara la Afrika, Tanzania ni moja ya nchi zinzonufaika na mpango huo ambao umesaidia kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu mikubwa.
“Afrika ni bara linalonufaika na mpango huu wa BRI, China haijawahi kutamani kutawala wengine,wao wanatafuta ushirikiano na kufanya biashara, ni masuala ya amani,umoja na maendeleo tu,”alisema Butiku.
Butiku alisema watoa mada wataeleza maendeleo ya ushirikiano huo wa mpango wa BRI, kwa nchi za Afrika Mashariki na kuainisha maeneo mengine yanayohitaji msukomo zaidi wa ushirikiano ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wa mataifa hayo.
“Tanzania imenufaika na mpango huu wa BRI, amani ,umoja na utulivu vimeendelea kunwa nguzo muhimu hata katika siasa tunapiga hatua kubwa ya ushirikiano na mataifa mengine hususan China, na hiyo imetusaidia kwa sababu kauli yetu siku zote ni amani na umoja zaidi,”alisema Butiku.
Alisema katika dunia ya sasa ushirikiano na mataifa mengine ni mambo ya msingi yanayohitajika zaidi hivyo mpango huo wa BRI ni fursa ya Tanzania na mataifa mengine ya Afrika Mashariki kuchangamkia kwa ajili ya maendeleo ya watu na mataifa yao.
No comments:
Post a Comment